Na Mwandishi Wetu, Moshi.
BARABARA zenye urefu wa kilomita 64 zilizojengwa kwa nguvu za wananchi na Wadau wa Maendeleo katika kijiji cha Kiruweni kata ya Mwika Kusini wilaya ya Moshi zipo hatarini kuharibika baada ya malori yenye vifaa vya ujenzi kuzitumia kama njia ya ukwepaji ushuru.
Baadhi ya malori ambayo hubeba vifaa hivyo ikiwemo mchanga, mawe, kokoto, na matofali kutoka wilaya ya Rombo eneo la Holili huzitumia kama njia ya ukwepaji wa ushuru wa halmashauri na pia kukwepa kupitia katika mizani.
Mwenyekiti wa kitongoji cha Kiruweni kati Jackson Machang'u amesema kuwa ipo haja ya mamlaka husika kuangalia upya jambo hilo kwani linasababisha hasara mara mbili ikiwemo kuharibu barabara lakini pia kuikosesha halmashauri mapato.
Amesema kuchelewa kudhibiti malori hayo kunaenda kuleta athari kubwa zaidi ikiwemo kuharibu barabara hizo zilizojengwa kwa nguvu za wananchi kwani hubeba mzigo mkubwa tofauti na viwango vilivyowekwa kisheria.
"Ipo haja ya mamlaka zinazohusika sasa kuona hili tatizo kwa sababunkwa siku sio chini ya malori 60 hadi 70 yanapita hivyo inaweza kuona ni nanma gani tatizo lilivyo kubwa katika eneo letu hili'amesema
John Tarimo diwani wa kata ya Mwika Kusini amesema kuwa tayari ameshapata malalamiko hayo na kuwa tayari ameshayafikisha kwa mamlaka husika ili kuweza kuchukuliwa kwa hatua kabla athari hazijawa kubwa zaidi ya hivi sasa.
Amesema ukweli ni kuwa barabara hizo zinapoharibika tatizo litabaki palepale kama ilivyo kuwa mwanzoni na kuwa kama sehemu ya kijiji hawezi kukubali kuona jitihada za wanançhi hao zinakwamisha kwa maslahi ya watu wachache
'Ikumbukwe tulitumia muda na fedha nyingi katika mradi huu wa barabara sasa maslahi ya wachache yasituharibie na kuturudisha kule tulipotoka mwanzoni'amesema
Mwisho.





0 Comments