SERIKALI YAJIPANGA KUTOA CHANJO YA HOMA YA INI KWA WATZ WOTE.

 


SERIKALI imesema inaendelea na maandalizi ya kuweka utaratibu wa kutoa chanjo ya homa ya ini kwa Watanzania wote, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kudhibiti na kutokomeza ugonjwa huo nchini.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, leo Aprili 10, 2026 bungeni jijini Dodoma, wakati akijibu swali la Mbunge wa Buchosa, Erick James Shigongo, katika Bunge la 13, Mkutano wa 3, Kikao cha 6 aliyetaka kujua Je ni lini Serikali itatoa chanjo ya Homa ya Ini kwa Watanzania Wote?.

Akijibu kwa niaba ya Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, Dk. Samizi amesema kwa sasa chanjo ya homa ya ini inatolewa kwa watoto wachanga kama sehemu ya ratiba ya taifa ya chanjo, ambapo hupatiwa muda mfupi baada ya kuzaliwa.

Ameongeza kuwa chanjo hiyo pia hutolewa kwa makundi maalum yaliyo katika hatari zaidi, ikiwemo watoa huduma za afya pamoja na makundi mengine yenye uwezekano mkubwa wa kuambukizwa.

“Chanjo ya homa ya ini inapatikana katika hospitali za Taifa, Kanda, Mikoa, pamoja na hospitali zote za Wilaya na Halmashauri. Mwananchi hupimwa kwanza na endapo hana virusi vya homa ya ini aina B hupewa chanjo hiyo kwa dozi tatu katika vipindi tofauti,” amesema Dkt. Samizi.

Aidha, amesema Wizara ya Afya imeunda timu ya wataalamu kwa ajili ya kuandaa andiko litakaloonesha mwelekeo pamoja na makadirio ya gharama za utekelezaji wa mpango wa kutoa chanjo hiyo kwa Watanzania wote.

Amesisitiza kuwa baada ya kukamilika kwa andiko hilo, Serikali itaanza hatua za utekelezaji wa mpango huo ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi wananufaika na huduma hiyo muhimu ya kinga.

Mwisho.

Post a Comment

0 Comments