Dawa za Pamba zinazotolewa na Bodi ya Pamba kwa ajili ya kudhibiti wadudu wanaoshambulia zao la pamba.Na COSTANTINE MATHIAS, Bariadi.
CHAMA Cha Wanunuzi wa Pamba Tanzania (TCA), kimepokea chupa mil. 8 za dawa ya kuuwa wadudu wanaoshambulia zao la pamba ambazo zimetolewa na serikali kupitia Bodi ya Pamba Tanzania (TCB) kwa ajili ya kusambazwa Kwa wakulima.
Imeelezwa kamba hadi sasa chupa Mil.6 zimesambazwa kwa wakulima wa Pamba nchini kwa lengo la kudhibiti wadudu wanaofyonza na kutafuna vitumba vya pamba.
Akizungumza leo na waandishi wa Habari za Pamba, Katibu wa Chama Cha Wanunuzi wa Pamba (TCA), Boaz Ogolla amesema kuwa kipindi hiki ni muhimu kwa Wakulima kwa ajili ya kudhibiti wadudu wanaoharibu zao la pamba ambapo asilimia kubwa ya Pamba huharibiwa na wadudu.
Ameeleza kwamba wadudu waharibifu wanaharibu matawi na matunda ambapo sasa serikali imekuja na Mkakati Maalumu kwa ajili ya kudhibiti wadudu kwa kutumia Teknolojia ndege nyuki, Maboza na Matrekta.
"Sisi kama Wanunuzi wa Pamba tunashiriki kufikisha dawa za Pamba kwa wakulima kutoka Bohari ya dawa na Mwanza na kupeleka Vijiji, tunahakikisha vijana wa BBT wanatoa Elimu ya kutosha kwa wakulima ili upuliziaji uweze kufanyika kwa usahihi, Elimu na jinsi ya kupulizia, vijana wanatoa Elimu" amesema na kuongeza.
Katibu wa Chama Cha Wanunuzi wa Pamba (TCA), Boaz Ogolla akiongea na waandishi wa Habari za Pamba.
"Jumla ya chupa Mil. 8 tutapeleka vijijini, mpaka wiki jana tumepeleka chupa mil.6 ambazo zimewafikia wakulima vijijini...niipongeze Bodi ya pamba sababu viuwadudu vimewafikia wakulima kwa wakati"
Kuhusu wakulima wa Pamba hai, Ogolla amesema kuwa dawa asili (bio pest side) zimeshafikishwa kwa wakulima na shughuli ya kudhibiti wadudu inaendelea kwenye mashamba ya Wakulima.
Ameeleza kuwa Mifumo ya BBT imefanya kila mnunuzi wa Pamba apewe eneo la kuwekeza ili kuwasimamia wakulima kuongeza uzalishaji.
Amewataka wakulima kuendelea kupokea Elimu kupitia kwa Maafisa Ugani ambao wamerahisisha Upatikanaji wa takwimu na idadi halisi ya wakulima wa Pamba.
Ogolla ambaye pia ni Meneja wa Kiwanda cha kuchambua Pamba cha Alliance Ginneries amesema kuwa Tanzania ni nchi pekee yenye uzalishaji unaoongezeka mwaka hadi mwaka kutokana na serikali kusimamia Uwekezaji wa sekta ya pamba.
Amesitiza kuwa endapo serikali itajitoa kusimamia zao la pamba, basi zao hilo litakuwa linalimwa kiholela na litakufa, huku akisisitiza serikali kusimamia uwekezaji ili kuongeza tija ya pamba.
"Tukiondoa Uwekezaji tukaacha soko huria mkulima atakata tamaa na hatapata Pamba ya kutosha, sisi serikali imetutaka kushiriki kwenye uzalishaji ili kuongeza tija, serikali imekuja na Mbinu ya kutushirikisha kwenye uzalishaji" amesema.
Mwisho.


0 Comments