Na Mwandishi wetu, Bariadi
KUELEKEA Maadhimisho ya miaka 62 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anamringi Macha ameongoza Wananchi katika kufanya usafi wa Mazingira na mitaro ikiwa ni kutekeleza agizo la Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Mwigulu Nchemba kuadhimisha sherehe hizo kwa kufanya usafi wa mazingira.
Akiwa ameambatana na Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Simon Simalenga pamoja na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Bariadi Dr. Judith Ringia leo 25 April, wamefanya Usafi katika viunga vya Mji wa Bariadi kwa kusafisha mitaro ya Barabara.
Akizungumza baada ya zoezi la usafi, Macha amewataka wafanyabiashara na wananchi kuzingatia usafi katika maeneo yao yanayowazunguka kwa kuhakikisha uchafu unawekwa sehemu sahihi na kuepuka kufanya biashara maeneo ambayo ndiyo chanzo cha uchafu kwa mazingira yetu
Aidha ametoa maagizo kwa Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi kuhakikisha wanasimamia vyema usafi wa mazingira kwa kushirikiana na viongozi wa kata na mitaa kwa kuhakikisha usafi unafanyika kila siku katika mazingira na siyo kusubiri usafi wa mwisho wa mwezi kwa lengo la kuweka mazingira katika Hali ya Usafi na Salama.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Mhe.Simon Simalenga amesema watatumia sheria ndogo kwa wanaokaidi kutunza usafi wa mazingira hivyo kuhatarisha afya za wananchi ikiwepo magonjwa ya malipuko.
Mwisho.








0 Comments