Na Samwel Mwanga, Simiyu.
BAADHI ya wananchi katika mkoa wa Simiyu wamejikuta wakizama kwenye mzunguko wa madeni baada ya kukimbilia mikopo ya haraka kupitia simu janja hali inayofichua upande wa pili wa huduma hizi za kidijitali ambazo kwa nje huonekana kuwa suluhisho la haraka la fedha.
Wakizungumza April 26,2026 na Mwananchi digital wamesema kuwa licha ya urahisi wa kupata mikopo kupitia programu zilizopo kwenye simu hizo wengi wanashindwa kumudu marejesho kutokana na riba kubwa na muda mfupi wa kulipa, na hivyo kujikuta wakikopa tena ili kulipa deni la awali.
Daud Makula mkazi wa mji wa Mwanhuzi wikaya ya Meatu anasema kuwa alianza kuchukua mkopo wa Sh 20,000 kwa ajili ya kufungua biashara ya genge la vitu vidogo vya matumizi ya nyumbani lakini alichelewa kulipa sasa mkopo umeongezeka.
“Nilichelewa kulipa kwa sababu biashara haikuenda vizuri. Nilipoingia kwenye app, nikakopa tena ili kulipa ule wa kwanza. Sasa deni limefika zaidi ya Sh120,000,” anasema.
Anadai kila siku hupokea ujumbe wa kumkumbusha kulipa, wakati mwingine kwa lugha kali inayoongeza presha ya kisaikolojia.
Naye Agata Johnson mkazi wa mjini Maswa anasema kuwa mfumo huu wa kukopa mkopo mpya kulipia wa zamani umegeuka kuwa kawaida lakini alikataa kueleza kuhusu viwango halisi vya riba na adhabu za ucheleweshaji.
Kwa upande wake,Mary Fotunatus ambaye ni mkazi wa mjini Bariadi anasema kuwa kampuni za mikopo hutumia taarifa za simu zao kuwasiliana na ndugu au marafiki pale wanapochelewa kulipa.
Masumbuko Manjale ni mkazi wa Mwamapalala wilaya ya Itilima anasema kuwa mbali na mzigo wa kifedha pia madeni haya yameanza kusababisha migogoro ya kifamilia na msongo wa mawazo.
"Mie nashindwa kulala kwa hofu ya wadai na huu ujumbe wa kila siku wa kukumbushwa kulipa kunanifanya.nikose raha,"amesema.
Ngazi George ni mtaalam wa masuala ya fedha anasema kuwa hali hiyo inatokana na ukosefu wa elimu ya fedha.
“Wananchi wengi wanavutiwa na urahisi wa kupata pesa bila kuangalia gharama zake. Mwisho wa siku wanajikuta wamenasa,” anasema.
Masunga Daud ni Mwanasheria wa kujitegemea anasema iwapo madai hayo ni ya kweli, basi kuna uwezekano wa ukiukwaji wa haki ya faragha.
“Ni muhimu kufahamu masharti kabla ya kutumia huduma hizi. Lakini pia mamlaka zinapaswa kuchunguza mwenendo wa kampuni hizi,Tatizo hili linaanza kuwa kubwa. Inahitaji elimu ya fedha kwa haraka ili kuwasaidia wananchi hasa vijana kufanya maamuzi sahihi,” anasema.
Anasema kuwa wakati mikopo ya fedha kupitia makampunibya smu za mkononi ikiendelea kuwa suluhisho la haraka kwa mahitaji ya fedha, hali halisi maeneo ya vijijini inaonyesha kuwa bila elimu ya fedha na udhibiti madhubuti, huduma hizi zinaweza kuwa mtego unaowasukuma vijana kwenye umaskini badala ya kuwainua kiuchumi.
"Nashauri kuwepo kwa kampeni za kitaifa za elimu ya fedha pamoja na ufuatiliaji mkali wa kampuni zinazotoa mikopo kidijitali,"amesema.
Benki Kuu ya Tanzania imekuwa ikisisitiza umuhimu wa taasisi za kifedha kufuata sheria na taratibu, lakini bado wananchi wengi hawajui ni kampuni zipi zimeruhusiwa rasmi kutoa mikopo hiyo.
Mwisho.


0 Comments