Makala ya Elimu: WALIMU WA KUJITOLEA WANAVYOZIBEBEA SHULE MZIGO KIMYA KIMYA.


Na Samwel Mwanga, Simiyu.

SAA1:30 asubuhi, kabla hata wanafunzi hawajafika shuleni, Mwalimu Asha (Siyo jina lake halisi) tayari yupo darasani akifuta ubao na kuandaa mada ya siku. 

Tofauti na walimu wengine walioajiriwa, yeye hana ajira ya serikali, ni mwalimu wa kujitolea anayelipwa kwa makubaliano ya kijamii na wakati mwingine fedha kidogo kutokana na michango ya wazazi na wakati mwingine hakuna chochote.

Uchunguzi wa Mwandishi wa makala kutoa SAKAGOI BLOG katika baadhi ya shule za Msingi na Sekondari za kata mbalimbali za mkoa wa Simiyu umebaini kuwa walimu wa kujitolea wamekuwa nguzo isiyoonekana katika kuendesha masomo, wakiziba pengo la upungufu mkubwa wa walimu walioajiriwa rasmi.

Baadhi ya Walimu Wakuu na Wakuu wa shule wanasema kuwa kwa wastani idadi ya walimu wa kujitolea kuwa ni kati  ya walimu 3 hadi 8 wa kujitolea hupatikana katika kila shule yenye upungufu mkubwa.

Katika baadhi ya shule za sekondari za kata, hadi nusu ya walimu wanaofundisha masomo ya sayansi na hesabu si waajiriwa wa serikali.

“Mwalimu mmoja wa serikali hawezi kufundisha madarasa yote. Tunategemea sana walimu wa kujitolea,” anasema Mkuu wa shule moja ya sekondari kata wilaya ya Meatu (jina limehifadhiwa).

Wanalipwaje? Mfumo usio rasmi, malipo yasiyo na uhakika

Tofauti na walimu wa ajira rasmi, walimu wa kujitolea hawana mshahara wa kudumu. Uchunguzi unaonyesha mifumo ifuatayo ya malipo michango ya wazazi (Shilingi 10,000–Sh30,000 kwa mwezi kwa baadhi ya shule).

Posho ndogo kutoka kwa kamati za shule na wengine hufundisha bila malipo wakisubiri ajira.

Mwalimu  Dastan Mayingu wa kujitolea katika wilaya ya Itilima anasema kuwa pamoja na kazi kubwa anayofanya lakini analipwa sh 50,000 au asilipwe kabisa.

“Unafundisha mwezi mzima, mwisho wa siku unaweza kupewa Sh50,000 au hata usipewe chochote. Lakini unaendelea kwa matumaini ya ajira.”anasema.


Kwa nini wanafundisha bila ajira?

Sababu kuu zilizobainika:

Ukosefu wa ajira rasmi kwa wahitimu wa ualimu matumaini ya kupata ajira baadaye,

shinikizo la jamii kusaidia shule zisizokuwa na walimu wa kutosha.

Davis Lema ni Mtaalamu wa elimu kutoka taasisi binafsi anasema hali hii imekuwa mfumo mbadala usiotambuliwa rasmi lakini unaoendesha elimu vijijini.


Athari kwa ubora wa elimu.

Hili ndilo eneo nyeti zaidi uchunguzi unaonyesha madhara yafuatayo kukosekana kwa uthabiti wa ufundishaji

Walimu wa kujitolea huondoka ghafla wanapopata fursa nyingine, hivyo wanafunzi hubaki bila mwendelezo wa masomo.

Motisha ndogo kutokana na malipo duni, na baadhi yao hukosa ari ya kufundisha kwa ubora wa juu.

 Upungufu wa mafunzo endelevu walimu hawa hawapati mafunzo rasmi ya serikali mara kwa mara, tofauti na walioajiriwa.

Mzigo mkubwa kwa wanafunzi katika baadhi ya shule darasa linaweza kubadilisha walimu mara 2 au 3 kwa mwaka katika somo moja.

Mariamu Mussa ni wanafunzi wa kidato cha tatu katika shule moja ya kata  katika wilaya ya Maswa anasema kuwa kubadilika mara kwa mara  kwa walimu katika kufundisha masomo kunawaathiri kitaaluma.

“Tunaanza topic na mwalimu mmoja, akiondoka anakuja mwingine anaanza upya au anafundisha tofauti.”anasema.

Walimu wa kujitolea: mashujaa au wahanga?

Wakati jamii inawanufaika, walimu hawa pia ni waathirika kwa kuwa wanakosa ajira rasmi kwa muda mrefu,wanakosa haki za msingi kama bima ya afya,wanaish maisha ya sintofahamu na baadhi yao wamefundisha kwa zaidi ya miaka mitatu bila ajira.


Serikali yasemaje?

Kwa mujibu wa sera za elimu, ajira ya walimu hutolewa kupitia taratibu rasmi za serikali. Hata hivyo, kasi ya ajira imekuwa ndogo kulinganisha na mahitaji halisi mashuleni.

Wadau wa elimu wanaitaka serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuongeza ajira za walimu na kuweka mfumo rasmi wa muda kwa walimu wa kujitolea ili kulinda haki zao na kuhakikisha ubora wa elimu.

Walimu wa kujitolea ni mfumo unaoishi kimya kimya uchunguzi huu unaonyesha kuwa walimu wa kujitolea si suluhisho la muda mfupi tena bali wamekuwa sehemu ya kudumu ya mfumo wa elimu vijijini

Swali linabaki: je, taifa linaweza kuendelea kutegemea mfumo usio rasmi kuendesha elimu ya watoto wake?

Bila hatua za haraka za kuongeza ajira na kuweka utaratibu wa wazi, kuna hatari ya kuendelea kushuka kwa ubora wa elimuwakati mzigo mkubwa ukiendelea kubebwa na walimu wasiotambulika rasmi.

Mwisho.


Mwisho.

Post a Comment

0 Comments