Na Mwandishi Wetu, Moshi.
BAADA ya wadau wa Maendeleo na nguvu za wananchi wa kijiji cha Kiruweni kilichopo katika kata ya Mwika Kusini kufanikisha Ukarabati wa barabara korofi zenye urefu wa zaidi ya kilomita 64 sasa wamehamua kuongeza nguvu katika kukarabati wa shule kongwe.
Imeelezwa kuwa, jtihada hizi zimeonesha nia ya dhati katika kuleta maendeleo sambamba na kuunga mkono serikali kwa miradi mbali mbali inayoitekeleza kwenye maeneo mbalimbali.
Diwani wa Kata ya Mwika Kusini, John Tarimo, anasema kuwa jitihada hizo ni maono ya wananchi hao na kuwa yeye kama kiongozi hana budi kuhakikisha ndoto zao za maendeleo zinatimia na kuwa huo ndio pia mpango wa serikali.
'Wananchi wanataka maendeleo na sio maneno na utaona miradi mbalimbali wanavyotekeleza kwa nguvu zao wenyewe hii ni ishara kuwa wana muamko wa maendeleo na mimi nipo nao bega kwa bega'asema
Kwa mujibu wa Tarimo ni kuwa maendeleo ni lazima yaletwe na wananchi wenyewe na kuwa bado michango ya hali na mali inahitajika kama walivyoianzisha ili malengo yao yaweze kutumia.
Martha Shayo mkazi wa kijiji cha Mawanjeni anasema ni muda sasa kwa wananchi kujitolea katika miradi ya maendeleo badala ya kusubiri wahisani ambapo hata hivyo haijulikani watakuja lini na kwa masharti gani.
'Kama tunavyochangia harusi au send off tuwe na moyo huo huo katika maendeleo yetu maana hapa ndio kwetu na kama ni shida tunazijua sisi wenyewe'" anasema.
Wadau hao wa maendeleo wameendelea kujitolea kama ilivyokuwa kwa mradi wa barabara ambapo kwa sasa baadhi ya shule kongwe zimeonekana kukarabatiwa hali inayojenga mazingira rafiki ya upatikanaji na utoaji wa elimu.
Baadhi ya shule hizo ni pamoja na shule ya msingi Mawanda yenye jumla ya wanafunzi 75 ambapo ukarabati wa ofisi ya walimu unaendelea pamoja na uwekaji sakafu kwenye baadhi ya vyumba vya madarasa.
Upo mradi wa ujenzi wa choo cha walimu katika shule ya msingi Karoro ambapo hapo awali walimu wapatao 6 walilazimika kutumia choo kimoja na wanafunzi.
Kadhalika ujenzi wa bweni la wasichana katika shule ya sekondari Mangi Marialle unaendelea kwa sasa ambapo kwa kukamilika kutakwenda kuondoa adha ya wanafunzi wa kike kutembea umbali mrefu unaowaingiza katika vishawishi na hatimaye kutofanya vizuri katika masomo yao.
Mwisho.







0 Comments