WATOTO 162,099 MASWA KUPATIWA CHANJO YA MATONE YA POLIO.

Mkuu wa wilaya ya Maswa, Dk Vicent Anney (kulia) akitoa chanjo ya matone ya.polio kwa mtoto wakati wa uzinduzi wa zoezi hilo wilayani humo.Picha na Samwel Mwanga

 Samwel Mwanga, Maswa.

Mkuu wa Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu, Dk Vincent Anney, amewataka wazazi na walezi kuhakikisha watoto wote wenye umri wa kuanzia miaka sifuri hadi 10 wanapatiwa chanjo ya matone ya polio ili kuwalinda dhidi ya ugonjwa huo unaoweza kusababisha ulemavu wa kudumu.

Akizungumza leo Machi 242026  wakati akizindua rasmi kampeni ya utoaji wa chanjo ya polio wilayani humo, ambapo jumla ya watoto 162,099 wanatarajiwa kufikiwa katika zoezi hilo.

Amesema utoaji wa chanjo hiyo ni hatua ya tahadhari baada ya kubainika kuwepo kwa kirusi kinachosababisha ugonjwa wa polio katika moja ya mikoa ya kanda ya Ziwa.

Kutokana na hali hiyo, amesema serikali imeamua kutoa chanjo katika mikoa sita ambayo ni Simiyu, Mara, Mwanza, Geita, Shinyanga na Singida ili kuzuia uwezekano wa kusambaa kwa ugonjwa huo.

Mkuu wa wilaya ya Maswa, Dk Vicent Anney akizungumza wakati wa uzinduzi wa chanjobya polio katika wilaya hiyo.Picha na Samwel Mwanga.

“Naomba niwatoe hofu wananchi, hakuna mtu aliyepatikana na ugonjwa wa polio. Baada ya kufanya vipimo kwenye maji, ilionekana kuna vimelea vinavyoweza kusababisha ugonjwa huo, ndipo serikali ikaamua kuchukua tahadhari kwa kutoa chanjo,” amesema.

Amesisitiza kuwa chanjo hiyo ni salama na haina madhara yoyote kwa watoto.

“Chanjo hii haina madhara yoyote kwa mtoto, na hata mtoto akipewa matone haya hatapata maumivu wala kulia,” amesema.

Kwa mujibu wa Mratibu wa chanjo wilaya ya Maswa, Abel Machibya amesema kuwa zoezi hilo litafanyika katika vituo 401 vilivyoandaliwa wilayani humo, huku vituo 39 vikiwa katika hospitali ya wilaya hiyo ambavyo vitahudumia maeneo jirani na mji wa Maswa.

Amesema lengo ni kuhakikisha watoto wote wenye umri husika wanapatiwa chanjo hiyo ili kuimarisha kinga dhidi ya ugonjwa wa polio.

Anastela Celestine ambaye ni muuguzi wa hospitali ya wilaya ya Maswa akitoa chanjo ya matone ya polio kwa wanafunzi wa shule ya msingi Binza.Picha na Samwel Mwanga.


Mkazi wa Maswa, Maria Aron, amesema hatua hiyo ni muhimu kwa ustawi wa watoto na kuwataka wazazi kuhakikisha wanawapeleka watoto wao kupata chanjo.

“Tunashukuru Serikali kwa kutujali. Nawashauri akina mama wote wenye watoto wenye umri husika kuwapeleka kupata chanjo hii muhimu,” amesema.

Kwa upande wake, Pili James amesema ugonjwa wa polio ni hatari kwa sababu unaweza kusababisha kupooza kwa mtoto, hivyo ni vyema wazazi kuhakikisha watoto wao wanapata chanjo mapema.

“Ni ugonjwa hatari sana. Hakuna mzazi anayependa kuona mtoto wake anapooza, hivyo chanjo hii ni muhimu sana,” amesema.

Baadhi ya wakinamama waliojitokeza katika hospitali ya wilaya ya Maswa iki watoto wao wapate chanjo ya ugonjwa wa polio.Picha na Samwel Mwanga

Naye Mratibu wa Chanjo kutoka Shirika la Msalaba Mwekundu Tanzania, Boniface Mabonedho, amesema taasisi yao inashirikiana na Serikali kuhakikisha zoezi hilo linafanikiwa na kila mtoto anayestahili anapatiwa chanjo.

Amesema timu za wahudumu wa afya na wadau wengine zimeandaliwa kuwafikia watoto katika vituo vilivyopangwa pamoja na maeneo ya jamii ili kuhakikisha hakuna mtoto anayekosa chanjo.

Kampeni hiyo ya chanjo ya matone ya polio itafanyika kwa siku nne, kuanzia Machi 24 hadi Machi 27, 2026, katika maeneo mbalimbali ya wilaya ya Maswa.

Mwisho.

Post a Comment

0 Comments