SAMIA ARDHI KLINIKI, CHACHU YA KUPUNGUZA MIGOGORO YA ARDHI SIMIYU.


Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Anamringi Macha (kulia) akikabidhi hati miliki ya ardhi kwa mmoja wa Wanawake waliohudhuria katika uzinduzi wa Samia Ardhi Kliniki iliyofanyika uwanja wa CCM mjini Bariadi.


 Samwel Mwanga, Simiyu.

 UZINDUZI  wa kliniki ya ardhi maarufu kama Samia Ardhi Kliniki umeelezwa kuwa ni chachu ya kupunguza migogoro ya ardhi mkoani Simiyu na faraja kwa vyombo vya utoaji haki, hususan mahakama.

 Akizungumza  Machi 4,2026 mjini Bariadi wakati wa uzinduzi huo,  Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania masijala ndogo ya Simiyu,Husein Mtembwa amesema kuanzishwa kwa kliniki hiyo kutasaidia kupunguza mlundikano wa mashauri yanayotokana na migogoro ya ardhi, ambayo imekuwa ikichangia kwa kiasi kikubwa kesi katika mahakama za mkoa huo..

 

Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Anamringi Macha (kulia) akimkabidhi hati miliki ya ardhi, Pendo Shija (kushoto) wakati wa uzinduzi wa Samia Ardhi Kliniki katika mkoa huo.

“Sehemu kubwa ya mashauri tunayopokea yanahusu migogoro ya ardhi. Kupitia kliniki hii, wananchi watapata elimu na usuluhishi wa mapema kabla ya kufikia hatua ya kufungua kesi mahakamani,” amesema.

 Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi wa Ardhi mkoa wa Simiyu, Denis Rugemalira, amesema lengo la Samia Ardhi Kliniki ni kuamsha chachu kwa wananchi, hususan wanawake, kujitokeza kumiliki ardhi kisheria.

 

Kamishna msaidizi wa ardhi mkoa wa Simiyu, Denis Rugemalira akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa uzinduzi wa Samia Ardhi Kliniki mkoani humo.

Amesema mkoa huo umejiwekea lengo la kutoa hati miliki 3,000 kwa mwaka, lakini hadi sasa hati 1,441 ndizo zimetolewa, kati ya hizo 405 ni za wanawake sawa na asilimia 28 pekee.

 

Baadhi ya wananchi wa mkoa wa Simiyu waliojitokeza wakati wa uzinduzi wa Samia Ardhi Kliniki mkoani huo latika mjini Bariadi.

“Tunahitaji kuona uwiano wa umiliki wa ardhi kati ya wanaume na wanawake unakuwa sawa. Bado wanawake wanamiliki ardhi kwa kiwango kidogo ukilinganisha na wanaume,” amesema.

Akifungua rasmi kliniki hiyo ya siku sita, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anamringi Macha, amesema lengo kubwa ni kuwapatia wanawake elimu kuhusu umiliki na usimamizi wa ardhi ili waweze kudai na kulinda haki zao.

“Mfumo dume bado upo kwa kiwango kikubwa katika baadhi ya maeneo ya mkoa wetu. Tunataka kuona wanawake wanapewa kipaumbele katika kushughulikia changamoto za ardhi na wanapata haki yao ya kumiliki mali,” amesema.

Pendo Shija, mkazi wa Maswa ambaye amepatiwa hati miliki ya ardhi amesema kliniki hiyo imekuja wakati muafaka kwani wanawake wengi wamekuwa wakinyimwa haki ya kumiliki ardhi za familia.

“Mara nyingi ardhi inaandikishwa kwa jina la mume pekee. Mwanamke akifiwa au kuachika anakosa pa kuanzia. Kliniki hii itatusaidia kujua haki zetu,” amesema.

 

Baadhi ya wananchi wa mkoa wa Simiyu waliojitokeza wakati wa uzinduzi wa Samia Ardhi Kliniki mkoani huo latika mjini Bariadi.

Naye Victoria Zavala kutoka mjini Bariadi amesema migogoro mingi ya ardhi vijijini inatokana na ukosefu wa elimu.

 “Watu wanagombania mipaka au mirathi kwa sababu hawana hati. Serikali ikiendelea kutoa elimu na kurahisisha 0upatikanaji wa hati miliki, kesi zitapungua,” amesema.

 Stela Manyonyi ni mkazi wa wilaya ya Busega amesema kuwa Samia Ardhi Kliniki itakuwa suluhisho la kudumu la migogoro ya ardhi, kuongeza usawa wa kijinsia katika umiliki wa ardhi na kupunguza mzigo wa mashauri katika mahakama zilizoko katika mkoa huo.


MWISHO.

 

Post a Comment

0 Comments