Na Mwandishi wetu.
BODI ya Maji Bonde la Ziwa Victoria imepokea Mtambo mmoja (1) wa Uchimbaji visima kati ya mitambo mitano (5) iliyotolewa na Wizara ya Maji kupitia Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kwa lengo la kuimarisha ufanisi katika uchimbaji wa visima na ujenzi wa mabwawa katika eneo la Bonde la Ziwa Victoria.
Akikabidhi mtambo huo, Meneja wa RUWASA Mkoa wa Simiyu, Mhandisi Emmanuel Luswetula, amesema hatua hiyo itasaidia kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya maji na Uchimbaji wa visima pia kuimarisha huduma kwa wananchi.
Amesema awali mitambo hiyo ilikabidhiwa RUWASA, lakini sasa wanaikabidhi Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria ili iweze kutoa huduma ya kuchimba visima.
Luswetula amesema, Mtambo huo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuboresha upatikanaji wa maji safi na salama, hususani katika maeneo yanayokabiliwa na changamoto ya uhaba wa maji.
"Awali mitambo hiyo ilikabidhiwa kwetu RUWASA lakini sasa tunaikabidhi Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria, wataisimamia na kuiendesha kuchimba visima na baada ya visima kuchimbwa watavikabidhi RUWASA kwa ajili ya Uendeshaji, pia watachimba visima vya watu binafsi" amesema Luswetula.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria, Dkt. Renatus Shinhu, ameishukuru Wizara ya Maji pamoja na RUWASA kwa kuiwezesha Bodi hiyo kupata mtambo huo ambao utasaidia kuongeza ufanisi katika uchimbaji wa visima na ujenzi wa mabwawa katika maeneo mbalimbali ya bonde hilo.
Mtambo huo ni PRD Mounted Drilling Rig with Compressor PG 1100 wenye namba ya usajili STM 2483, uliounganishwa na compressor pamoja na vifaa vyake ambavyo ni Mud Pump, Welding Machine, pamoja na gari saidizi (Support Truck) lenye namba ya usajili STM 2444, ambalo hutumika kubeba na kusaidia uendeshaji wa vifaa vya mtambo huo wakati wa utekelezaji wa majukumu.
Mwisho.




0 Comments