KIHONGOSI AWATAKA WAKULIMA WA PAMBA SIMIYU KUACHANA NA KILIMO CHA KIZAMANI.

 

Katibu Mwenezi wa CCM Taifa, Kenan Kihongosi (aliye kati) akizungumza mara ya baada ya kukagua shamba la pamba katika kijiji cha Mwatumbe wilaya ya Maswa. Picha na Samwel Mwanga

Samwel Mwanga,Maswa.

KATIBU wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Kenan Kihongosi, amewataka wakulima wa zao la pamba katika mkoa wa Simiyu kuachana na kilimo cha kizamani na badala yake kuzingatia kilimo cha kisasa ili kuongeza uzalishaji kwa kila hekari.

Kihongosi alitoa kauli hiyo leo Machi 7,2026 alipokuwa akikagua shamba la pamba la mkulima John Moga, mkazi wa kijiji cha Mwatumbe wilayani Maswa, ambapo alieleza kuwa serikali imeweka mazingira rafiki ya kuongeza tija katika zao hilo.

Amesema kwa sasa serikali kupitia Bodi ya Pamba Tanzania imeanza kutoa pembejeo kwa wakulima ikiwemo mbegu bora, viuadudu pamoja na teknolojia ya kisasa ya ndege nyuki kwa ajili ya kunyunyizia dawa katika mashamba makubwa ya pamba bila gharama kwa mkulima.

“Serikali imeleta teknolojia ya kisasa ya ndege nyuki ambayo inasaidia kunyunyizia viuadudu kwenye mashamba makubwa kwa haraka bila gharama kwa mkulima, hivyo inapunguza muda na nguvu zinazotumika kuhudumia shamba,” amesema.


Ndege nyuki ikimwagilia dawa ya kuua wadudu katika shamba la pamba katika kijiji cha Mwatumbe wilaya ya Maswa huku akishuhudia Katibu Mwenezi wa CCM Taifa, Kenan Kihongosi (hayupo pichani).Picha na Samwel Mwanga.

Kwa upande wake mkulima huyo, John Moga, amesema uamuzi wa serikali kulisimamia zao la pamba kwa kutoa pembejeo umewasaidia wakulima kuongeza uzalishaji kwa kiasi kikubwa.

Amesema hapo awali walikuwa wakivuna wastani wa kilo 300 kwa hekari moja lakini kwa sasa uzalishaji umeongezeka hadi kufikia kilo 1,000 kwa hekari kutokana na matumizi ya mbegu bora na kufuata ushauri wa wataalamu wa kilimo.

Mbunge wa Jimbo la Maswa Magharibi, Mashimba Ndaki, amesema kwa sasa wakulima wa pamba wameanza kunufaika na zao hilo kutokana na jitihada za serikali kuwapatia pembejeo bure na elimu ya kilimo bora.

Hata hivyo alimwomba Katibu Mwenezi wa CCM Taifa kuendelea kuishauri serikali kuangalia suala la bei ya pamba ili wakulima waweze kunufaika zaidi na jasho lao.

“Elimu uliyotupa leo itatufaa zaidi kwa wakulima wetu, hasa wanaolima zao la pamba. Tunaomba pia suala la bei liendelee kufanyiwa kazi ili wakulima wapate faida zaidi,” amesema.


Shamba la pamba la mkulima John Moga, mkazi wa kijiji cha Mwatumbe wilaya ya Maswa lililotembelewa na Katibu Mwenezi CCM Taifa,Kenan Kihongosi.Picha na Samwel Mwanga.

Naye Mkuu wa Divisheni ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Hassan Kiseto, amesema maafisa ugani katika wilaya hiyo kuanzia ngazi ya kijiji hadi kata wanaendelea kuwafikia wakulima kwa kuwapatia elimu ya kilimo bora cha pamba.

Amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha wakulima wanatumia mbinu sahihi za kilimo ili kuongeza uzalishaji na kipato chao.


Mkuu wa Divisheni ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Hassan Kiseto (aliyenyoosha mikono) akitoa maelezo kwa Katibu Uenezi CCM Taifa,Kenan Kihongosi (wa tatu kushoto) jinsi shamba hilo la pamba lilivyolimwa kwa kufuata kanuni bora za kilimo cha zao hilo.Picha na Samwel Mwanga.

Shaban Mwandila, mkulima  wa kijiji cha Mwatumbe amesema kuwa teknolojia ya kunyunyuzia dawa zao la pamba imewarahisishia kazi wakulima.

“Teknolojia ya kunyunyizia dawa kwa kutumia ndege nyuki imerahisisha kazi. Zamani tulitumia muda mwingi kunyunyizia dawa kwa mkono lakini sasa inafanyika haraka na mashamba yanapata dawa kwa usawa.”amesema

Naye Maria Nyambalya, mkulima wa kijiji cha Shishiyu wikayani humo amesema mbegu bora za pamba na pembejeo ni kichocheo kwa wakulima kulima zao hilo.

“Mbegu bora na pembejeo zinazotolewa na serikali zimetusaidia sana. Kama bei ya pamba itaendelea kuboreshwa, wakulima wengi zaidi watahamasika kulima zao hili.”amesema.

Kwa upande wake mkulima,Paulo Mwanajeje  wa kijiji cha Mwaliga amesema kuwa maafisa ugani wamekuwa msaada mkubwa sana kwao.

"Elimu ya maafisa ugani imekuwa msaada mkubwa. Tunajifunza namna ya kulima kwa mistari, kutumia mbegu bora na kupambana na wadudu waharibifu, hivyo uzalishaji unaongezeka.”amesema.


Mwisho.

Post a Comment

0 Comments