CCM KUHAKIKISHA PAMBA INANUFAISHA WAKULIMA.



Na Mwandishi wetu.


CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kitaendelea kuisimamia na kuisisitizia serikali kuhakikisha bei ya Pamba inamnufaisha mkulima.


Katibu wa Halmashauri Kuu Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kenani Kihongosi ameeleza hayo alipotembelea mradi wa Shamba la Pamba lililopo katika Kijiji cha Mwantumbe Kata ya Shishiyu Wilayani Maswa Mkoa wa Simiyu.


Kihongosi amesema Mkoa wa Simiyu unatambulika kwamba Pamba ni dhahabu nyeupe, Pamba ni uchumi, Pamba ni fedha, hivyo wataibeba ajenda ya wakulima wa Pamba na mazao mengine yakiwemo Tumbaku na waweze kuona tija katika kilimo, kwani kilimo ni uti wa mgongo wa taifa.


“Na sisi tutazidi kuisisitiza serikali kama chama kwa kuhakikisha bei ya pamba inamnufaisha mkulima, hili tutalibeba kama ajenda ili wakulima wa Pamba na mazao mengine yakiwemo Tumbaku na kadhalika waweze kuona tija katika kilimo,” amesema Kihongosi.


Ameongeza kuwa serikali imejaribu teknolojia nzuri, imewashughulikia na kuwajali wakulima kwa kilimo cha kisasa na kitaalamu, lengo ni kuendelea kuachana na kilimo cha zamani.


Amesema kazi ya chama ni kusimamia utekelezaji wa Ilani, kwa sababu haya yanayoonekana na kufanyika yapo ndani ya Ilani yao ya uchaguzi ya mwaka 2025/30 kwamba watakwenda kuboresha kilimo na kuboresha miundombinu yake.


Mwisho. 

Post a Comment

0 Comments