PAMPU 1,000 ZAPELEKWA KISHAPU, DC ATIA NENO.


MKUU wa Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga, Peter Masindi (kulia) akikabidhi pampu ua kupulizia dawa kwa mmoja wa wakulima wa Kijiji cha Mihama kata ya Lagana wilayani humo, kushoto ni Mkaguzo wa Pamba wilaya hiyo, Joackim Gobanya.



Na COSTANTINE MATHIAS, Kishapu.


SERIKALI kupitia Bodi ya Pamba Tanzania (TCB) imegawa pampu 1,000 kwa wakulima bora wa Pamba wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga kwa ajili ya upuliziaji ili kudhibiti wadudu katika msimu wa kilimo 2025/2026.


Aidha wakulima hao wametakiwa kuzingatia kanuni 10 za kilimo cha pamba pamoja na maelekezo ya wataalamu ili waongeze uzalishaji, wajikwamue kiuchumi na wakuze pato la Taifa.



Hayo yamebainishwa leo na Mkuu wa Wilaya hiyo, Peter Masindi wakati akikabidhi pampu hizo pamoja na kuona unyunyiziaji wa Pamba kwa kutumia ndege zisizo na rubani katika mashamba ya wakulima kwa lengo la kuwarahisishia shughuli za kilimo.



Masindi aliwataka wakulima kufuata kanuni za kilimo bora cha pamba ikiwemo kukata masalio, kupanda kwa mistari, kupalillia kwa wakati, kunyunyizia dawa ili waweze kuvuna kwa tija.


Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga, Peter Masindi (aliyesimama) akiongea na wakulima wa Kijiji cha Mihama wakati akikabidhi pampu kwa ajili ya kupulizia pamba.


"Fateni kanuni za kilimo, kateni masalio, Serikali imeleta solo pampu ambazo zitaenda kwa wakulima 1000 ili wakatumie kwenye uzalishaji wa pamba...Serikali inawekeza ili kukusaidia, usipotunza unajikomoa mwenyewe, tunataka madawa yatumike vizuri na msiyauze" alisema na kuongeza.


"Tutumie vifaa hivyo sababu ni vya muhimu sana ambavyo vitatutoa sehemu moja kwenda nyingine, tuwatumie wataalam wa BBT ili wawasaidie katika utaalamu, Tunahitaji kila mkulima ekari moja apate kilo 1000, Kishapu ibebwe na Pamba, hakikisha kila kaya Ina Pamba."  


Alisema kuwa Bodi ya Pamba wanafanya kazi kubwa sana ya kuwahudumia wakulima ili waweze kufanikiwa huku serikali ikitaka mkulima aweze kuinuka kiuchumi kupitia shughuli za kilimo.

MKUU wa Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga, Peter Masindi (kulia) akikabidhi pampu ya kupulizia dawa kwa wakulima wa Kijiji cha Mihama kata ya Lagana wilayani humo, kushoto ni Mkaguzo wa Pamba wilaya hiyo, Joackim Gobanya.


Diwani wa Kata ya Mwamashele wilayani Kishapu, Lucas Daud aliipongeza Bodi ya Pamba kuja na Teknolojia ambazo zimerahisisha shughuli za kilimo kwa wakulima.


Alisema kupitia vikao vya Madiwani, wanahimiza wakulima kuzingatia kanuni za kilimo cha pamba ili kuongeza uzalishaji na kwamba serikali inategemea ushuru wa zao la pamba ili kuendesha shughuli kila siku pamoja na kutekeleza miradi ya Maendeleo.


Juma Paul Njile, mkulima wa Pamba Kijiji cha Lwagalalo kata ya Mwamashele wilayani humo alisema awali alikuwa akilima kwa kuchanganya na mazao mengine lakini baada ya kupata Elimu ameongeza uzalishaji kutoka kilo 150 na kufikia kilo zaidi ya 900 kwa ekari moja.



"Kuchanganya Mahindi na Pamba hakuna tija, Nilitumia nguvu kubwa na gharama kubwa kulima kwa kuchanganya mazao...nimeona faida na tija, mwaka jana nilivuna kilo 974 kwa kila ekari moja baada ya kuacha kuchanganya mazao, nawashauri wakulima wawe wasikumivu, wafuate kanuni za kilimo za Pamba, wafuate ushauri wanaopewa na wataalamu" alisema.



Mwisho.










Post a Comment

0 Comments