MASWA YAKABIDHIWA GARI LA ZIMAMOTO NA UOKOAJI.

 

Mkuu wa mkoa wa Simiyu,Anamringi Macha (mwenye shati jeupe) akikata utepe ikiwa ni ishara ya kukabidhi gari la Zimamoto na Uokoaji katika wilaya ya Maswa.


Samwel Mwanga,Maswa.

Jeshyi la Zimamoto na Uokoaji katika wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu,limepewa mtambo wa kuzima moto wenye uwezo wa kufika kwenye jengo lenye urefu wa ghorofa 10 ikiwa ni sehemu ya mkakati wa serikali kukabidhi mitambo hiyo kwa ajili ya shughuli za jeshi hilo katika wilaya zote nchini.

Akikabidhi gari hilo jumatano,Februari 18,2026 mjini Maswa,Mkuu wa mkoa wa Simiyu,bAnamringi Macha amesema kuwa kukabidhiwa kwa mtambo huo wa kuzimia moto ni juhudi za  serikali katika kulipatia jeshi hilo vitendea kazi ili liweze kutekeleza majukumu ya kila siku.

Amesema kuwa mojawapo ya malalamiko ya wananchi kuhusu jeshi hilo ni uhaba wa vitendea kazi lakini serikali imeliona hilo na ndiyo maana imekabidhi mtambo huo ambao ni mpya.

Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Anamringi Macha akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi gari la Zimamoto na Uokoaji katika wilaya ya Maswa.

“Huu ni mfano wa kuigwa,tangu wilaya ya Maswa kuanzishwa ni miaka 100 ilikuwa haina gari au mtambo wa kuzima moto huu ni mfano wa kuigwa,serikali inaendelea kushughulikia changamoto za jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa kununua mtambo kama huu,”amesema.

Amesema kuwa ni vizuri wakala wa barabara mjini na vijijini (Tarura) wakahakikisha miundo mbinu ya barabara inakuwa vizuri ili gari hilo liweze kufika mahali popote katika wilaya hiyo pindi litakapohitajika,

Kaimu Mkuu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoa wa Simiyu,Faustine Mtitu amesema kuwa ni vizuri kwa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Mjini Maswa(Mauwasa) na Wakala wa Maji na usafi wa Mazingira vijijini (Ruwasa) kutenga vituo vya kujazia maji ili kuwezesha gari hilo linapoishiwa maji kuyapata umbali wa mita 100 mjini na umbali wa mita 200 vijijini.

Kaimu Mkuu wa jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoa wa Simiyu,Faustine Mtitu akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi gari la Zimamoto na Uokoaji wilaya ya Maswa.

‘Gari hili lenye thamani ya zaidi ya Sh 2.3 bilioni ni vizuri wananchi wakalitumia kwa kutoa taarifa ya majanga yanapotokea nasi tutafika kwa wakati huu ni mtambo ukiwa na vifaa vya kisasa vya kuthibiti moto na kuokoa maisha ya watu na mali zao,”amesema.

Mkuu wa wilaya ya Maswa,Dk Vicent Anney amesema wilaya hiyo imekuwa ikikumbwa na majanga ya moto kwa muda mrefu na upatikanaji wa gari hilo ni hatua ya kihistoria.

Mkuu wa wilaya ya Maswa, Dk Vicent Naano akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhiwa gari la Zimamoto katika wilaya hiyo.

“Kupokea gari hili leo ni hatua kubwa na muhimu kwa wilaya yetu kongwe ambayo imeanzishwa miaka 100 iliyopita,litasaidia kusukuma kuwahudumia wananchi hasa watakapopata majanga ya moto,”amesema.

Anitha Mboje ni mkazi wa mjini Maswa amesema kuwa wilaya hiyo hiyo imepata mkombozi wa majanga ya moto kutokana na kuwepo kwa ajali za nyumba kuungua moto.

“Tumepata mkombozi gari hili limefika kwa wakati unaohitajika kwani majanga ya moto katika mji wa Maswa yamekuwepo ya mara kwa mara na watu wengi mali zao hupotea kwa kuteketea kutokana na mbinu duni za kuzima moto,”amesema.

MWISHO.

Post a Comment

0 Comments