KIHONGOSI AMWAGIZA DC IGUNGA KUKUTANA NA WACHINBAJI WADOGO.




Na Mwandishi wetu, Igunga.


KATIBU wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kenan Kihongosi, amemtaka Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Sauda Mtondoo, kukutana na kuwasikiliza wachimbaji wadogo wa madini wilayani humo ili kutafuta suluhisho la haraka na la haki kuhusu malalamiko yao.


Kihongosi ametoa agizo hilo leo wilayani Igunga alipokuwa akikagua mradi wa ujenzi wa shule ya awali na msingi Ibologero, akisisitiza kuwa chama na serikali hazitafumbia macho changamoto zinazowakabili wananchi, hususan wanaojitafutia kipato kupitia sekta ya madini.



Amesema ni wajibu wa uongozi wa wilaya kuhakikisha sauti za wachimbaji zinasikilizwa kwa makini na kufanyiwa kazi kwa kuzingatia sheria, taratibu na maslahi mapana ya taifa.


“Mkuu wa Wilaya afike, akae na wachimbaji, awasikilize na ajiridhishe na madai yao. Pale yatakapohitaji ngazi ya juu zaidi, hatua zichukuliwe kwa mujibu wa utaratibu,” amesema Kihongosi.


Amesisitiza kuwa serikali inalenga kuhakikisha sekta ya madini inanufaisha Watanzania wote, wakiwemo wachimbaji wadogo ambao wamekuwa wakichangia ajira na mzunguko wa fedha katika jamii.


Wito huo unakuja kufuatia malalamiko ya wachimbaji wadogo wanaodai kuingiwa na mwekezaji mkubwa katika maeneo ambayo tayari walikuwa wameanza kuyafanyia kazi, hali inayowatia hofu ya kupoteza vitega uchumi vyao.

Mwisho

Source;

#uhuruonline



Post a Comment

0 Comments