WAKATI serikali kupitia Bodi ya Pamba Tanzania (TCB) ikitangaza kuanza kwa soko huria la ununuzi wa Pamba katika msimu ujao wa 2026/2027, Wanunuzi wa Pamba wameunga mkono maelekezo hayo huku wakiahidi ushirikiano kuhakikisha mkulima anaongeza uzalishaji.
Akizungumza na waandishi wa Habari za pamba na Mazingira (TACOEJ), Katibu wa Tanzania Cotton Ginners (TCA), Boaz Ogolla alisema kuwa wamepokea Maelekezo ya ununuzi wa Pamba yaliyotolewa na Bodi ya Pamba kuwa na soko huria na kwamba wameshirikishwa katika maamuzi hayo.
Alisema kuwa Soko huria la zao la pamba siyo geni, kwani mfumo wa wanunuzi wengi uliingia nchini tangu mwaka 1994, lakini umekuwa ukifanyia Majaribio mara kwa mara ili kuona namna Bora ya kumkomboa mkulima ikiwemo kuongeza bei ya Pamba.
"Tulifanya kujaribu kusimamia baadhi ya maeneo, lakini tumeona hitaji la wakulima ni kuwa Soko huria, Serikali ni sikivu na angalifu, Wanunuzi wanaangalia mahitaji yote ili kufikia bei ya mkulima...kuna ushindani wakati wa kununua, ukikumbuka Mwaka jana na mwaka juzi tulianza kununua kwa tenda za kimataifa na soko likianguka, hata tukinunua kwa bei nafuu hatuwezi kuuza katika soko la Dunia" alisema.
Alieleza kuwa wazo la soko huria wamelipokea kwa moyo mazuri na kama itatokea nafasi ya ushindani, watashindana kwa bei inayofahamika kwenye soko la Dunia na kwamba utaratibu wa upangaji bei utaonekana ili mkulima anufaike na jasho lake.
"Mfumo wa mnunuzi mmoja umelalamikiwa na wakulima na serikali ikaona, na sisi tulishirikishwa kwenye maamuzi na tukaunga mkono, Tuendelee na mfumo unaokubalika il kila mmoja anufaike na kufurahia, ili sekta ya pamba iwe na utulivu wa kutosha.
Kuhusu usambazaji wa mbegu za pamba, Ogolla aliipongeza Bodi ya Pamba Kwa kusambaza mbegu kwa wakati wakishirikiana na wanunuzi na wakulima wako tayari kuanza kupanda huku akiwasisitiza wakulima kuzingatia maelekezo ya wataalamu wa Kilimo.
Alisema zao la pamba ni zao lenye soko la uhakika na kuwasisitiza Wakulima kulima Pamba ili iweze kuwaondoa kwenye umaskini endapo watazalisha kwa tija.
Alisema uzalishaji wa utaalamu umenufaisha wakulima huku aliwataka wadau mbalimbali waendelee kujikita kumpa elimu mkulima.
"Ukipeleka mahitaji yote lakini kama hakuna Elimu haitakuwa manufaa, Wakulima wanaopokea mbegu, wazingatie viipimo wakati wa upandaji, wapande kwa mstari, ukimwaga zigizaga hata kupitisha trekta itakuwa ngumu...wazingatie upandaji unaoelekezwa na BBT." Alisema.
Mwisho.



0 Comments