
MKUU wa Mkoa wa Simiyu, Said Mtanda (wa pili kushoto) akikabidhi jezi ikiwa ni sehemu ya uzinduzi wa ligi ngazi ya Mkoa wa Simiyu.
Na COSTANTINE MATHIAS, Bariadi,
MKUU wa Mkoa wa Simiyu, Said Mtanda, ameielekeza Halmashauri ya Mji wa Bariadi kuhakikisha wanaboresha Uwanja wa Michezo wa Halmashauri hiyo kwa kutenga bajeti, hatua inayolenga kuimarisha na kukuza shughuli za michezo mkoani humo.
Mtanda ametoa agizo hilo leo wakati akizungumza na wananchi pamoja na viongozi wa Chama Cha Mpira wa miguu Mkoa huo (SIFA) kwenye uzinduzi wa Ligi ya Mkoa wa Simiyu uliofanyika katika uwanja huo, ambapo amesisitiza umuhimu wa kuwa na miundombinu bora ya michezo inayoweza kuwasaidia wanamichezo kufanya vizuri.
Amesema maboresho ya uwanja huo ni muhimu katika kuweka mazingira rafiki kwa wanamichezo, mashabiki pamoja na wadau mbalimbali wa michezo, huku yakichangia kuongeza hamasa na ushiriki wa wananchi katika shughuli za michezo.
"Kwenye Bajeti ya Halmashauri mwakani, na mimi ndio niaeidhinisha Bajeti za Halmashauri zote na ndio nitakayekwenda kusoma bajeti ya mkoa wa Simiyu kule Dodoma, kipengele kimoja wapo ambacho nataka ikiwemo kwenye Bajeti ni kuboresha Uwanja wa Halmashauri" amesema na kuongeza.
"Lazima tuwe na vyumba vya kisasa vya kubadilisha nguo, kuanzia sasa nimeshapiga marufuku vibanda hapo nyuma kuanzia mwakani wekeni kwenye Bajeti ili tuboreshe Uwanja hu ulioko katikati ya Mji".
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amesisitiza kuwa uwekezaji katika miundombinu ya michezo ni sehemu ya juhudi za kukuza vipaji vya vijana, kuwawezesha kushiriki katika mashindano mbalimbali na kutumia michezo kama njia ya kujenga afya, nidhamu na mshikamano katika jamii.
Awali, Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Simiyu (SIFA), Osuri Kosuri, alisema ligi hiyo ya Mkoa wa Simiyu inashirikisha timu 14 yenye vijana kutoka ndani ya Mkoa wa Simiyu.
Alisema kuwa tangu Mkuu huyo wa Mkoa kuteuliwa, wakazi wa Mkoa wa Simiyu wana maratajio makubwa sana na uongozi wake katika sekta ya Michezo, hivyo watashirikiana nae kukahikisha wanakuza vipaji vya vijana kupitia Michezo ya Mpira wa miguu.
Uzinduzi wa Ligi ya Mkoa ni hatua muhimu katika kuendeleza michezo mkoani Simiyu, huku agizo la kutenga bajeti ya maboresho ya uwanja likitarajiwa kuwa chachu ya kuboresha mazingira ya michezo na kuongeza ushindani kwa timu zinazoshiriki ligi hiyo.
Timu ya Pamba Jiji Fc kutoka jijini Mwanza imecheza mechi ya kirafiki na Timu ya Simiyu Combine katika uzinduzi wa ligi hiyo ambapo pia Mkuu wa Mkoa huo alitimiza ahadi yake ya kutoa jezi ni mipira kwa timu 14 ambazo zitashiriki mashindano hayo ya kusaka bingwa wa Mkoa.
Katika mchezo huo, uliovuta hamasa Kwa mashabiki wengi wa soka mjini Bariadi, Pamba Jiji iliibuka Mshindi wa goli 2-0 dhidi ya Simiyu Combine.
0 Comments