POLISI, TAKUKURU WAREJESHA MILIONI 348 ZA MIKOPO MASWA.


Mkuu wa wilaya ya Maswa,Dk Vicent Naano akizungumza katika hafla ya utoaji wa mikopo ya asilimia 10 kwa makundi maalum kupitia halmashauri ya wilaya hiyo.

 Na Samwel Mwanga, Maswa.

JESHI la Polisi kwa kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Maswa, mkoani Simiyu, limefanikiwa kurejesha Sh348 milioni kati ya Sh700 milioni zilizokopeshwa kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kupitia mpango wa mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Fedha hizo zimekusanywa kutoka kwa wanufaika waliokuwa wamekopa na kushindwa kurejesha kwa wakati, baada ya operesheni iliyowezesha zaidi ya watu 30 wa vikundi mbalimbali kukamatwa. Hadi sasa, Sh352 milioni bado hazijarejeshwa.

Mkuu wa divisheni ya maendeleo ya jamii,halmashauri ya wilaya ya Maswa,Hollo Ngeme akitoa taarifa ya hali ya utoaji wa mikopo kwa makundi maalum wilayani humo.

Akizungumza Novemba 17, 2026, wakati wa kukabidhi mikopo ya Sh110 milioni kwa vikundi 12 vya makundi maalumu, Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dk Vicent Naano, amesema serikali itaendelea kuwachukulia hatua watu wote waliokopa fedha hizo na kushindwa kurejesha kwa mujibu wa masharti yaliyowekwa.

Amesema fedha zinazotolewa kupitia mpango huo si hisani, bali ni mikopo inayolenga kuwawezesha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kujikwamua kiuchumi, hivyo ni wajibu wa wanufaika kurejesha kwa wakati ili kutoa fursa kwa wengine.

"Fedha hizi si za mtu binafsi wala si hisani ya serikali. Zimetolewa kwa ajili ya kuwawezesha wananchi kiuchumi, hivyo kila aliyekopa anapaswa kurejesha kwa wakati ili wengine nao wapate nafasi ya kunufaika na mpango huu," amesema.

Dk Naano amewataka wananchi ambao bado hawajapata mikopo hiyo kujiunga katika vikundi na kuomba mikopo, akieleza kuwa halmashauri ina Sh100 milioni ambazo bado hazijapata wakopaji.

Ameiagiza halmashauri hiyo kuhakikisha fedha hizo zinatolewa kwa vikundi vinavyokidhi vigezo ndani ya wiki mbili kuanzia Novemba 17, 2026.

Sehemu ya wanachama wa vikundi mbalimbali kupitia makundi maalum wakiwa katika hafla ya utoaji wa mikopo katika halmashauri ya wilaya ya Maswa.

Amesema mikopo hiyo haina riba, hivyo ni fursa kwa makundi maalumu kuanzisha na kuendeleza shughuli za uzalishaji mali badala ya kutegemea mikopo yenye masharti magumu inayotolewa na baadhi ya wakopeshaji mitaani maarufu kama kaushadamu.

Kwa upande wake, Mkuu wa Divisheni ya Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Hollo Ngeme, amesema katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2026/2027, halmashauri imetoa Sh110 milioni kwa vikundi 12 vilivyokidhi vigezo vya kupata mikopo hiyo.

Amesema kati ya fedha hizo, Sh100 milioni zimetokana na mgao wa asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri, huku Sh10 milioni zikitokana na marejesho ya mikopo iliyotolewa awali.

"Vikundi 10 vya wanawake vimekopeshwa Sh85.1 milioni, kikundi kimoja cha vijana kimepata Sh21 milioni na kikundi kimoja cha watu wenye ulemavu kimepata Sh3.9 milioni,"amesema.

Amesema miongoni mwa sababu zinazochangia baadhi ya wanufaika kushindwa kurejesha mikopo kwa wakati ni matumizi yasiyoendana na malengo ya miradi waliyoainisha wakati wa kuomba fedha hizo.

Amesema ni muhimu wanufaika kuhakikisha fedha wanazopata zinatumika katika shughuli walizoziomba ili ziweze kuzalisha mapato yatakayowawezesha kurejesha mikopo na kuendeleza biashara zao.

Katika hatua nyingine, baadhi ya wanufaika wa mikopo hiyo wamesema fedha walizopata zitawasaidia kuongeza mitaji na kupanua shughuli zao za kiuchumi.

Wande Samson, mwanachama wa kikundi cha wanawake cha Mkombozi kilichopo kijiji cha Mwabalaturu, amesema kikundi hicho kinachojihusisha na kuongeza thamani ya zao la mpunga kitatumia mkopo huo kuongeza mtaji ili kuboresha shughuli zake na kuongeza ufanisi katika biashara.

Naye Letisia Sumuni, mwanachama wa kikundi cha Mamalishe kilichopo kata ya Isanga, amesema mkopo huo utamwezesha kuongeza idadi ya kondoo wa asili anaowafuga, hatua itakayopanua biashara yake ya nyama na kuongeza kipato kupitia uuzaji wa kondoo na mbegu zao.

Kwa upande wake, Mwajuma Josephat, mkazi wa kijiji cha Nghami ambaye ana ulemavu wa ngozi, amesema mkopo huo utamuwezesha kununua cherehani na kuanza kujiajiri kupitia taaluma ya ushonaji aliyopata katika chuo cha mafunzo ya ufundi stadi jijini Mwanza.

Amesema licha ya kuwa na ujuzi wa ushonaji, alishindwa kuanza kazi hiyo kutokana na ukosefu wa mtaji wa kununua mashine ya kushonea nguo.

"Nimepata mafunzo ya ushonaji, lakini changamoto ilikuwa mtaji wa kununua cherehani. Kupitia mkopo huu nitanunua mashine na kuanza kazi yangu ili niweze kujipatia kipato. Nitajitahidi kurejesha fedha hizi kwa wakati," amesema.

Catherine Daniel, mwanachama wa kikundi cha Amani na Upendo kilichopo mjini Maswa, amesema utaratibu wa kupata mikopo hiyo uko wazi na unatoa fursa kwa vikundi vinavyokidhi vigezo bila upendeleo.

Amewahimiza wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kujiunga katika vikundi ili waweze kutumia fursa hiyo kujikwamua kiuchumi.

Mwisho.




Post a Comment

0 Comments