Na COSTANTINE MATHIAS, Bariadi.
MKUU wa Mkoa wa Simiyu, Said Mtanda amesema kuwa ameridhishwa na Kasi ya ujenzi wa kituo cha kupozea Umeme kinachojengwa katika Mtaa wa Imalilo, Halmashauri ya Mji wa Bariadi Mkoani Simiyu.
Akizungumza mara baada ya Kukagua ujenzi wa kituo hicho, Mtanda amesema ujenzi wa Mradi huo umefikia asilimia 80 na serikali imeshatoa fedha zote kwa ajili ya kituo hicho ambacho kinajengwa na mkandarasi wa ndani.
"Fedha za ujenzi wa kituo shilingi Bil. 8 zipo kwenye akaunti, serikali Iko kazini na mradi huo ukikamilika utamaliza tatizo la kukatika Kwa umeme.. Mahitaji ni Megawati 17.5 lakini kituo hiki kikikamilima tutazalisha Megawati 54, wanasimiyu hawatakuwa na changamoto ya Umeme" amesema Mtanda.
Amemtaka Meneja wa Tanesco Mkoa Simiyu kuhakikisha anasimamia fedha hizo ili ifikapo mwezi Oktoba 2026 kituo hicho kiwe kimekamilika.
Meneja wa Tanesco Mkoa wa Simiyu, Twaha Kigangama amesema kuwa ujenzi wa kituo cha Umeme umefikia asilimia 80, pia kuna ujenzi wa njia ya kusafirishia Umeme kutoka Ibadakuli (Shinyanga) kuja Bariadi ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 60.
Amesema kuwa ujenzi wa Mradi huo unatekelezwa na Wakandarasi wawili ambapo kituo cha kupozea Umeme kinagjarimu shilingi Bil.8 na njia ya kusafirishia Umeme inajengaa kwa gharama ya Shilingi Bil. 55.
Msimamizi wa Mradi wa Ujenzi wa kituo cha kupozea Umeme, Mhandisi Daniel Kato amesema kuwa Utekelezaji wa Mradi huo ulianza kutekeleza Oktoba 2025 na wanatarajia kukamilisha ifikapo Oktoba 2026.
"mradi una hatua mbili, hatua ya kwanza ni ujenzi wa njia ya Msongo wa kilovoti 220 ambao unaendelea na hatua ya pili tunajenga kituo cha kupozea Umeme na tutaweka mashine umba (Transfoma) ya MVA 60 sawa na Megawati 60 na tutakuwa na matoleo ya njia nane" amesema Mhandisi Kato.






0 Comments