MTANDA; "NIMEKUJA KUFANYA KAZI SIMIYU, SITAKI UFALME WALA UCHAWA".

MKUU wa Mkoa wa Simiyu, Said Mohamed Mtanda akizungumza na Watumishi wa Mkoa huo mara baada ya kuwasili Kwa ajili ya kuanza kazi.


Na COSTANTINE MATHIAS, Bariadi,

MKUU wa Mkoa wa Simiyu, Said Mohamed Mtanda, amewataka Viongozi, Watumishi wa umma na wananchi wa mkoa huo kumpa ushirikiano katika utekelezaji wa shughuli za maendeleo, akisema ameteuliwa katika nafasi hiyo kwa ajili ya kufanya kazi na si vinginevyo.

Ametoa kauli hiyo wakati leo, Sept 4, 2027, wakati akizungumza na wananchi na viongozi mbalimbali mara baada ya kuanza majukumu yake mkoani Simiyu, akimshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kumuamini na kumpa nafasi ya kuongoza mkoa huo.

Amesema kuwa amefika Simiyu akiwa na dhamira ya kushirikiana na wananchi na viongozi kuhakikisha shughuli za maendeleo zinatekelezwa kwa ufanisi.

“Nimekuja Simiyu kufanya kazi...Naomba ushirikiano katika shughuli za maendeleo, kiongozi hapimwi kwa ukubwa wa eneo analoliongoza, bali kwa utekelezaji wa shughuli za maendeleo,” amesema.

Mtanda amesema uzoefu alioupata ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Serikali utamsaidia kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia masilahi ya wananchi.

Amesema katika utumishi wa umma amejijenga katika misingi ya uwazi, ukarimu na kutokwamisha watu katika utekelezaji wa majukumu yao.

“Katika utumishi wa umma mimi ni mtu muwazi, mkarimu na sipendi kukwamisha...nafanya kazi bila kukwamisha, Sitaki kumfitini mtu, sitaki UCHAWA , napenda kusema ukweli, ingawa kwa bahati mbaya Watanzania hatupendi ukweli,” amesema.

Amesema kuwa akiwa kiongozi yuko tayari kukosolewa na kujadiliwa, akisisitiza kuwa mijadala inapaswa kulenga mambo yenye manufaa kwa jamii badala ya kushambulia watu binafsi.

“Ukiwa kiongozi ni lazima usemwe na ujadiliwe. Napenda watu wanaojadili mambo ya maana na si mtu,” amesema.

Mtanda pia amewatoa hofu wananchi kuhusu aina ya uongozi wanaopaswa kuutarajia kutoka kwake, akisema hataki kujenga makundi ya watu wanaomzunguka kwa maslahi binafsi.

“Niwahakikishieni mimi sina chawa. Umri wa kuchaguliwa marafiki kwa sasa haupo,” amesema.

Amesema anaamini katika kufanya kazi kwa utaratibu na kwa muda mrefu badala ya kutafuta mafanikio ya haraka kwa njia zisizo sahihi.

“Mimi si mtu wa deal wala si mtu wa kutafuta deal. Ninaamini katika utendaji wa kazi. Nimechagua kula kidogo kidogo ila kwa muda mrefu,” amesema.

Akemea Rushwa, wizi.

Mkuu huyo wa mkoa amesema hatakuwa tayari kuvumilia vitendo vya wizi wa fedha za umma na rushwa, akitaka wananchi wapewe nafasi ya kushiriki katika shughuli za maendeleo.

“Wizi wa fedha mimi si mvumilivu, pamoja na vitendo vya rushwa. Tuwapatie wananchi nafasi,” amesema.

Amesema atashirikiana na viongozi na watendaji katika ngazi mbalimbali, lakini hatakuwa tayari kutumia muda na nguvu za Serikali katika mambo yasiyo na msingi.

“Tufanye kazi kwa ushirikiano. Mimi siko tayari kufanyia kazi mambo ambayo hayana msingi,” amesema.

Milango iko wazi.

Mtanda amesema Ofisi ya Mkuu wa Mkoa itakuwa wazi kwa wananchi, akisema hawatalazimika kupitia taratibu ngumu za kuomba miadi ili kufikisha kero, changamoto au mapendekezo yao.

“Nawahakikishia wananchi kuwa milango iko wazi kwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa. Hakuna kuwekeana appointment,” amesema.

Amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha wananchi wanapata nafasi ya kueleza changamoto zao na kushiriki katika kujenga mkoa huo.

Nimezoea maisha ya vijijini’.

Mtanda amesema licha ya kuwa kiongozi wa Serikali, amezowea maisha ya vijijini na kwamba ana mtazamo wa kuendelea kuishi maisha hayo hata baada ya kumaliza safari yake ya uongozi.

“Nimezoea maisha ya kuishi vijijini na fikra zangu, nikiachana na uongozi nitakaa vijijini,” amesema.

Kauli hiyo imekuja wakati akisisitiza umuhimu wa viongozi kuwa karibu na wananchi na kuelewa changamoto zinazowakabili katika maisha yao ya kila siku.

Ampongeza DC Maswa.

Katika hatua nyingine, Mtanda amempongeza Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dkt Vicent Anney, kwa hatua aliyoanzisha ya kutengeneza madawati kwa ajili ya kupunguza tatizo la wanafunzi kukaa chini katika shule za wilaya hiyo.

Amesema juhudi kama hizo zinapaswa kuungwa mkono kwa sababu zinaelekeza nguvu katika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi, hususan katika sekta ya elimu.

Mtanda amewataka viongozi wa mkoa huo kuendelea kubuni na kutekeleza mipango yenye matokeo yanayoonekana katika maisha ya wananchi.

Amesisitiza kuwa maendeleo ya Simiyu yatahitaji umoja, ushirikiano na uwajibikaji wa viongozi pamoja na wananchi.

Mwisho.










Post a Comment

0 Comments