Na Mwandishi wetu.
JESHI la Polisi Mkoa wa Simiyu, limefanikiwa kumpata kijana mmoja aitwaye Gatami Maduhu Martine miaka 20, Msukuma na Mkazi wa Kijiji cha Mwauchumu Wilaya ya Bariadi, anayedaiwa kutoweka katika mazingira ya kutatanisha kwa muda wa wiki moja na kuibua hofu kwa familia amepatikana.
Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi mkoani humo, imeelezwa kuwa, Mnamo tarehe 25/09/2026 majira ya saa 10.00 jioni Jeshi la Polisi lilipokea taarifa kutoka kwa Gatami Maduhu Maltine (64) Msukuma, Mkazi wa Mwauchumu, akieleza kuwa, Mjukuu wake aitwaye Gatami Maduhu Martine, aliondoka tangu tarehe 19/09/2026 na kwenda Mgodini huko Mwabasabi Kata ya Gibeshi na tarehe 23/09/2026 Majira ya 4.00 usiku Gatami Maduhu, alimpigia simu mdogo wake aitwaye Sayi Maduhu kwa kupitia namba 0613 035 688 na kumweleza kuwa, yupo sehemu hajui ni wapi na ana siku ya tano (5) yupo ndani ya nyumba amefungiwa na watu hao wanaodaiwa kumteka wanataka watumiwe pesa kiasi cha shilingi milioni tano (5,000,000) ili wamwachie.
Baada ya taarifa hizo kupokelewa kituo cha Polisi Bariadi Jalada la uchunguzi lilifunguliwa na ufuatiliaji wa taarifa hizo ulianza mara moja kupitia timu ya makachero kwa kushirikiana na ndugu wa kijana huyo ambapo walifanikiwa kumpata Gatami Maduhu Martine akiwa huko Kata ya Bwanga Wilaya ya Chato Mkoa wa Geita akiwa mzima wa afya bila tatizo lolote.
Aidha, Jeshi la Polisi linaeleza kuwa, uchunguzi kuhusiana na tukio hilo umebaini kuwa Gatami Maduhu Martine alijiteka kwa nia ya kupata pesa toka kwa ndugu zake huku likitoa wito kwa wananchi kuacha tabia hii ya kujipatia kipato kwa njia ya udanganyifu kwani matukio ya namna hii yanajenga taharuki kwa jamii na kwamba mtu yeyote atakaye jaribu kufanya hivyo atakamatwa na sheria itachukua mkondo wake.
Mwisho.

0 Comments