DC MASWA AMALIZA MGOGORO WA ARDHI ULIODUMU MIAKA 30.


Mkuu wa wilaya ya Maswa, Dk Vicent Naano akizungumza na wananchi wa kata ya Shanwa juu ya kumalizika kwa mgogoro wa ardhi katika ya wananchi hao na Seminari ya Shanwa. Picha na Samwel Mwanga.


Na Samwel Mwanga, Maswa.

MGOGORO wa ardhi uliodumu kwa miaka 30 kati ya wananchi wa Kata ya Shanwa, wilaya ya Maswa, mkoa wa Simiyu na Seminari ya Shanwa ya Kanisa Katoliki, Jimbo la Shinyanga, umetatuliwa baada ya wananchi 174 kupatiwa viwanja kwa ajili ya makazi.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya Kanisa Katoliki kukubali kuachia sehemu ya eneo lenye ukubwa wa ekari 104, huku serikali ikisimamia upimaji na ugawaji wa viwanja kwa wananchi.

Akizungumza Septemba 25, 2026, Mkuu wa wilaya ya Maswa, Dk Vicent Naano, amesema kuwa  suluhisho hilo limepatikana baada ya vikao vya pamoja vilivyowakutanisha Serikali, wananchi na kanisa Katoliki.

Amesema mgogoro huo ulianza mwaka 1996 baada ya kanisa kuchukua eneo hilo na kuwalipa fidia wananchi 22 waliokuwa wakiishi ndani ya eneo hilo, lakini baadhi yao hawakuondoka na waliendelea kufanya shughuli mbalimbali ikiwemo kilimo na ujenzi wa nyumba.

Mkuu wa wilaya ya Maswa, Dk Vicent Naano akiwaonyesha wananchi wa kata ya Shanwa boksi lililo na karatasi za namba za viwanja ambapo kila mwananchi mmoja atachukua karatasi moja ili aonyweshwe kiwanja chake. Picha na Samwel Mwanga.

“Mgogoro huu sasa umetimiza miaka 30, lakini leo hii nafurahi kuwajulisha kuwa katika vikao tulivyokaa kati ya viongozi wenu wananchi, kanisa Katoliki na serikali, tumekubaliana mgogoro huu uishe,” amesema.

Amesema kuwa wananchi watapangiwa viwanja katika eneo lililoachwa na kanisa, huku wale wenye makaburi wakitambuliwa na kuachwa maeneo hayo kwa utaratibu maalumu.

Amesema viwanja vitagawiwa kwa utaratibu wa bahati nasibu, ambapo kila mwananchi atachukua karatasi yenye namba kutoka kwenye boksi na baadaye kuonyeshwa eneo la kiwanja chake na kila mnufaika anapatiwa hati ya umiliki wa ardhi.

Hata hivyo, Dk Naano aliwaonya wananchi dhidi ya kuvamia eneo la kiwanja namba mbili ambacho bado ni mali ya kanisa na hakijaendelezwa.

Sehemu ya wananchi wa eneo la Shanwa wilaya ya Maswa waliohudhuria mkutano wa mkuu wa wilaya hiyo, Dk Vicent Naano (hayupo pichani) wa kugawiwa viwanja vya makazi. Picha na Samwel Mwanga.

“Tumekubaliana kuwa kiwanja namba mbili ni mali ya kanisa. Hakuna mtu yeyote kuvamia na atakayekwenda kinyume atakutana na mkono wa sheria. Hatuwezi kurudi tena kwenye mgogoro wa ardhi,” amesema.

Viwanja 181 vyapimwa.

Afisa Ardhi wa Wilaya ya Maswa, Vivian Christian, amesema eneo hilo limepimwa na kupatikana viwanja 181, ambapo 174 vitagawiwa wananchi kwa ajili ya makazi.

Alisema viwanja vilivyosalia vitatengwa kwa ajili ya taasisi za huduma za jamii, ikiwemo shule, kituo cha afya, kituo cha polisi na maeneo ya wazi.

Amesema kuwa mgogoro huo uliongezeka baada ya baadhi ya wananchi kufungua kesi mahakamani mwaka 2017, lakini walishindwa na baadaye wakaondolewa katika eneo hilo kwa nguvu.

“Wananchi walipoona eneo ambalo halijaendelezwa waliendelea kuvamia na wale waliolipwa fidia hawakuondoka, ndipo mgogoro ukawa mkubwa. Lakini kupitia vikao tumelimaliza vizuri na kila upande umeridhika,” amesema.

Amesema kuwa katika eneo hilo, kiwanja namba moja ndicho kilichoendelezwa kwa kujengwa seminari, huku viwanja namba mbili na tatu vikiwa havijaendelezwa.

Wananchi wasifu suluhisho.

Mkazi wa Shanwa, Paul Sambe, amesema kuwa viongozi kadhaa waliowahi kuwa wakuu wa wilaya walijaribu kutatua mgogoro huo bila mafanikio, akieleza kuwa moja ya changamoto ilikuwa wananchi kutoshirikishwa kikamilifu.

“Kuna wakuu wa wilaya wapatao watatu wamepita katika wilaya hii, lakini walishindwa kumaliza mgogoro huu. Leo hii Dk Naano kaumaliza. Hii ndiyo tafsiri ya uongozi wa kuyapatia suluhisho matatizo ya wananchi,” amesema.

Lumaza Chuma, aliyekuwa mwenyekiti wa kamati ya upimaji wa viwanja akiwakilisha wananchi, amesema kuwa uamuzi wa Kanisa Katoliki kuachia sehemu ya eneo hilo ni hatua inayopaswa kupongezwa.

“Taasisi ya dini imeonyesha kweli iko kwa ajili ya kuwasaidia wananchi. Kitendo walichokifanya Kanisa Katoliki kuachia sehemu ya ardhi ni cha kistaarabu na uamuzi wa busara,” amesema.

Kwa upande wake, Vicent Peter amesema mgogoro huo uliwaathiri wananchi kwa miaka mingi, akieleza kuwa baadhi yao walikamatwa na kuwekwa mahabusu, huku wengine wakiondoka katika familia zao kwa hofu ya kukamatwa na polisi kutokana na tuhuma za kuvamia eneo hilo.

Amesema kumalizika kwa mgogoro huo kumewapa wananchi fursa ya kupata maeneo rasmi ya makazi na kuondoa hofu iliyodumu kwa miaka mingi.

Mwisho.

Post a Comment

0 Comments