Mbunge wa jimbo la Maswa Magharibi,Mashimba Ndaki akizungumza katika mkutano wa hadhara katika Kata ya Mwabayanda.
Na Samwel Mwanga, Maswa.
MBUNGE wa Jimbo la Maswa Magharibi, Mashimba Ndaki, amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa kuhakikisha gulio la Mwabayanda linajengewa choo ifikapo Desemba 2026, baada ya kubainika kuwa wafanyabiashara wamekuwa wakilipa ushuru bila kupata huduma hiyo.
Ndaki alitoa agizo hilo Septemba 21,2026 katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kata ya Mwabayanda, uliolenga kusikiliza kero za wananchi na kutoa shukrani kwa wakazi wa eneo hilo kwa kumchagua yeye kuwa Mbunge, pamoja na kumchagua Rais na Diwani, wote kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Akizungumza katika mkutano huo, mkazi wa Mwabayanda, Masanja Martine, amesema kuwa gulio hilo hufanyika kila siku ya jumanne na limekuwa likitozwa ushuru na halmashauri, lakini halina choo kwa ajili ya wafanyabiashara na wananchi wanaofika kufanya shughuli za biashara.
Alisema hali hiyo imekuwa ikilazimisha baadhi ya watu kutumia maeneo ya wazi, jambo linaloweza kuhatarisha usafi na afya ya jamii.
Martine pia alieleza changamoto ya mto unaokatiza njia ya kuelekea shule ya msingi Mwabayanda, akiiomba serikali kujenga daraja ili kuwawezesha wanafunzi na wananchi kuvuka kwa usalama, hasa wakati wa mvua.
Kwa upande wa elimu alisema kuwa shule hiyo pia haina vyoo vya kutosha, hali inayowalazimu wanafunzi kujisaidia vichakani.
Akijibu hoja hizo, Ndaki alimuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa kuhakikisha choo kinajengwa katika gulio hilo kabla ya Desemba 2026 huku akisisitiza ya kuwa suala hilo liko ndani ya uwezo wa halmashauri.
Changamoto nyingine iliyowasilishwa katika mkutano huo ni ubovu wa barabara kutoka Ilamata hadi Mwabayanda ambayo tayari imeshaanza kufanyiwa matengenezo na mkandarasi tayari amekwisha kuanza kazi.
Mbunge Ndaki akizungumzia suala la umeme amesema kuwa kwa sasa vijiji vyote vya jimbo hilo vina umeme na sasa kazi iliyopo ni kupeleka umeme kwenye vitongoji.
"Ndugu zangu umeme sasa unafika kwenye vitongoji na ifikapo mwaka 2030 vitongoji vyote vitakuwa na umeme hivyo niwaombeni sana mvute umeme kwenye nyumba zenu na siyo nyaya za umeme tuzione zimepita kwenye nguzo tu,"amesema.
Katika hatua nyingine Mbunge Mashimba Ndaki ambaye anaendelea na ziara zake katika kata zote za Jimbo hilo amekuwa akigawa seti moja ya jezi na mpira mmoja wa miguu kwa kila kijiji ili kuunga mkono suala la michezo hususani mpira wa miguu.
Mwisho.







0 Comments