Na COSTANTINE MATHIAS, BARIADI.
MBUNGE wa Jimbo la Bariadi Mjini, Mhandisi Kundo Mathew ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maji amesema kuwa Wizara hiyo imejipanga kuhakikisha inatatua kero ya Maji katika Mkoa wa Simiyu kutokana na uwepo wa Mwezeshaji Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ambaye ametoa fedha za kujenga Mradi wa Maji kutoka Ziwa Viktoria ambao unagharimu shilingi Bil. 440.
Mhandisi Kundo ameyasema hayo jana mbele ya Waziri Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba kwenye Mkutano wa Hadhara uliofanyika katika Uwanja wa CCM mjini Bariadi ambapo alisema kuwa mradi huo utahudumia vijiji 103 na una urefu wa kilometa 400 na vituo vya kuchotea Maji 443.
"Tunaye Mwezeshaji Rais Dk. Samia ambaye ametoa fedha tutekeleze Mradi wa Maji kutoka Ziwa Victoria kwa gharama ya Shilingi Bil. 440, tumetoa tenda kwa mkandarasi Otonde kusambaza Mtandao wa mabomba ya Maji kutoka Busega (Kwa Songe), Bariadi vijijini (Kwa Kadogosa) hapa mjini mpaka Itilima (kwa Njalu)... Tunaenda kuhakikisha huduma ya Maji inaboreshwa na Wananchi wanapata Maji" amesema Mhandisi Kundo.
Licha ya kutekelezwa Mradi huo mkubwa ambao umefikia asilimia 72, Mhandisi Kundo amesema kuwa Serikali inaendelea kutekeleza miradi midogomidogo ikiwemo Mradi wa Maji Isanga unaotekelezwa kwa gharama ya Shilingi Bil. 1.2, Mradi wa Maji Guduwi, Nyakabindi, Bunamhala, Nyangokolwa, pamoja na Mradi kabambe kwenye kata nne za Mjini ambazo ni Somanda, Sima, Malambo na Bariadi.
Amesema kuwa miradi hiyo ikikamilika wananchi hawatakuwa na tatizo la Maji tena kwani Rais Dk. Samia Suluhu Hassan atakuwa amemaliza tatizo la Maji katika Jimbo la Bariadi Mjini.
Mwisho.







0 Comments