Sehemu ya mabenchi 13 yaliyotengenezwa na watumishi wa hospitali ya wilaya ya Maswa kwa ajili ya kukalia wagonjwa.Na Samwel Mwanga,Maswa.
WATUMISHI wa kada mbalimbali katika Hospitali ya Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu wamechangisha kiasi cha fedha Sh 938,000 kwa ajili ya kutengeneza mabenchi 13 kwa ajili ya kukalia wagonjwa na wananchi wanaofika hospitalini hapo kupata huduma za afya.
Hatua hiyo imekuja baada ya uongozi wa hispitali hiyo kubaini upungufu wa sehemu za kukalia wagonjwa kufuatia kuongezeka kwao pindi wanaofika hospitalini hapo kupata matibabu.
Akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya mabenchi hayo,Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya hiyo Dk Deogratias Mtaki amesema kuwa maamuzi hayo yalifikiwa katika kikao cha pamoja cha watumishi wote ambapo walikubalina kila mmoja kuchangia kiasi cha Sh 5000.
Amesema katika kufanikisha suala hilo iliundwa kamati maalum kwa ajili ya kusimamia michango hiyo pamoja na matumizi ambayo yalikusudiwa.
“Huu ni moyo wa kujitolea unaopaswa kuigwa. Watumishi wameonesha kuwa hata mchango mdogo wa kila mmoja unapounganishwa unaweza kuleta matokeo makubwa kwa taasisi na wananchi tunaowahudumia,” amesema.
Pia Dk Mtaki ametumia fursa hiyo kuwashukuru wote walioshiriki katika zoezi hilo huku akisisitiza mchango huo ni sadaka yao kwa taasisi na mfano wa uzalendo katika utumishi wa umma.
Baadhi ya wananchi waliofika hospitalini hapo wamepongeza hatua hiyo, wakisema itawasaidia wagonjwa na walezi wanaotumia muda mrefu kusubiri huduma.
“Kabla ya benchi hizi, wakati mwingine unakuta wagonjwa wengi wamesimama kwa sababu sehemu za kukalia hazitoshi. Hasa kwa wazee na wagonjwa wenye hali dhaifu, hali hiyo ilikuwa changamoto,” amesema Esther Elias mkazi wa Njiapanda mjini Maswa.
Naye Silvester Lugembe mkazi wa mtaa wa Unyanyembe amesema hatua hiyo imeonyesha mshikamano kati ya watumishi na wananchi wanaotumia huduma za hospitali hiyo.
“Tunawapongeza sana watumishi. Wameonyesha kuwa wanaweza kushirikiana kutatua changamoto zinazowagusa wananchi moja kwa moja. Benchi hizi ni msaada mkubwa kwa wanaokuja kupata huduma,” amesema.
Hospitali ya wilaya ya Maswa imekuwa ikipata wagonjwa wengi kutokana na kutegemewa na wananchi wa wilaya hiyo na baadhi ya wilaya jirani za Itilima na Meatu mkoani humo na wilaya ya Kishapu iliyopo mkoa wa Shinyanga.
Mwisho.



0 Comments