Na COSTANTINE MATHIAS, Bariadi.
WANAWAKE ambao ni Wakazi wa Mitaa ya Nyangaka, Kidinda na Buzunza kata ya Bariadi Halmashauri ya Mji wa Bariadi Mkoani Simiyu, wameiomba serikali kujengewa nyumba ya mtumishi, pamoja na wodi ya Wazazi kwa ajili kujifungulia ili waondokane na adha ya kutembea umbali mrefu kwenda Somanda na Muungano kupata huduma hiyo.
Wakizungumza jana August 1, 2026 kwenye Mkutano wa Hadhara, uliotishwa na Mbunge wa Jimbo la Bariadi Mjini, Mhandisi Kundo Mathew, wananchi hao wamesema zahanati ya Nyangaka inatoa huduma kwa wagonjwa wa nje na kwa nyakati za usiku hakuna huduma yoyote kutokana na ukosefu wa nyumba ya mtumishi.
Lucia Raphael, Mkazi wa Nyangaka aliipongeza serikali kwa kuwajengea zahanati lakini haitoi huduma nyakati za usiku pamoja na huduma ya wanawake kujifungua kutokana na kukosa wodi ya kujifungulia.
"wakina mama tunahangaika kwenda kujifungulia Somanda au Muungano kutokana na ukosefu wa nyumba ya mtumishi na wodi kwenye zahanati ya Nyangaka...tunaomba serikali Ione jambo hili muhimu maana tunashikwa na uchungu nyakati za usiku, tunalazimika kwenda Muungano au Somanda ambalo ni mwendo mrefu" amesema.
Limi Sayi, Mkazi wa Kidinda amesema kuwa endapo watajengewa nyumba ya mtumishi, huduma zitakuwa zinatolewa siku zote katika juma tofauti na sasa ambapo Jumamosi na jumapili hakuna huduma zinazoendelea.
Akizungumzia changamoto hiyo, Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi, Dr. Mohamed Omary, amekiri zahanati hiyo kukosa nyumba ya mtumishi pamoja na wodi ya wakinama kujifungulia ambapo aliahidi kuwa jambo hilo limeweka kwenye Bajeti ijayo Kwa ajili ya Utekelezaji.
Ameongeza kuwa, zahanati hiyo ilijengwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kupitia Mpango wa Kunusuri Kaya Maskini ambapo katika Bajeti yao hawakuwa na kipengele cha ujenzi wa Nyumba ya mtumishi na wodi ya kujifungulia akina mama.
Mbunge wa Jimbo hilo, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Mathew amewahakikishia wananchi kushughulikia kero hiyo kwa kupeleka maombi Maalumu wizarani kwa lengo la kupata fedha za ujenzi huo.
Mbunge wa Jimbo la Bariadi Mjini, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Mathew akiwasikiliza wananchi (hawapo pichani) wakiwasilisha kero zao kwenye Mkutano wa Hadhara uliofanyika kata ya Bariadi.
"Nitaenda wizarani kuomba pesa, tutakayoanza na kimoja wapo, tukaseme kimojawapo ili kipate majawabu...na Wananchi hawa waweze kupata huduma karibu na makazi yao na kwa nyakati zote" amesema.
Katika hatua nyingine, Mbunge huyo amesema atatafuta kiasi cha Shilingi Mil. 115 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa mradi wa maji, uliopo Mtaa wa Salunda ili kuongeza upatikanaji wa huduma ya Maji.
Amesema kuwa hatua hiyo, itaimarisha huduma kwa wananchi na itaondoa tatizo la mgao wa maji, linalowakumba wananchi wa eneo hilo, wakiwamo wanaoishi ukanda wa Malinoni.
Mwisho.




0 Comments