Na Mwandishi wetu.
JESHI la Polisi Mkoa wa Simiyu, kupitia Kikosi cha Usalama Barabarani na Polisi Jamii, limeendelea kuimarisha ushirikiano na jamii kwa kutoa elimu ya usalama na kuhamasisha upendo, huruma na mshikamano kwa watu wenye mahitaji maalum.
Elimu hiyo imetolewa Agosti 21, 2026, katika Shule ya Msingi Somanda ‘A’, iliyopo Mtaa wa Bomani, Kata ya Somanda, Wilaya ya Bariadi, na kuambatana na matendo ya huruma kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa wa Simiyu, Kamishna Msaidizi wa Polisi, (ACP) Asiago Ochieng, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na jamii katika kuzuia na kupambana na uhalifu, pamoja na kulinda makundi yenye mahitaji maalum.
ACP Ochieng amesema Jeshi la Polisi ni rafiki wa jamii na kwamba watoto wenye mahitaji maalum wanahitaji upendo, ulinzi, heshima na mazingira salama ili waweze kutimiza ndoto zao.
Amewahimiza wanafunzi na jamii kwa ujumla kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa kuhusu vitendo vya uhalifu na matukio yanayoweza kuhatarisha usalama katika jamii.
Mwisho.





0 Comments