‎ENG. KUNDO ASHIRIKI KUKABIDHI SHILING MIL. 222 ZA MIKOPO BARIADI MJINI.

Mbunge wa Jimbo la Bariadi Mjini ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Mathew (katikati), akikabidhi Mfano wa hundi ya mikopo ya asilimia 10 Kwa vikundi vya Vijana, Wanawake na Watu wenye Ulemavu wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi.

Na COSTANTINE MATHIAS, Bariadi.

‎HALMASHAURI ya Mji wa Bariadi Mkoani Simiyu imetenga na kukabidhi fedha kiasi cha shilingi Mil. 222 Kwa ajili ya mikopo ya   vikundi 22 vya Vijana, Wanawake na Watu wenye Ulemavu 2025/26 kutokana na fedha za Mapato ya ndani.

‎Mbunge wa Jimbo la Bariadi Mjini ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Mathew, ameshiriki katika hafla hiyo, huku akiwahimiza wanufaika kutumia mikopo hiyo kwa malengo yaliyokusudiwa ili kuanzisha na kuendeleza shughuli za uzalishaji zitakazoongeza kipato, kufungua fursa za ajira na kuboresha maisha yao pamoja na familia zao.

Mbunge wa Jimbo la Bariadi Mjini ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Mathew, akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi mikopo ya asilimia 10 Kwa vikundi vya Vijana, Wanawake na Watu wenye Ulemavu wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi.


Mhandisi Kundo amewataka Watendaji wa Halmashauri kutengeneza uwazi wa michakato ya kupata mikopo, kujenga usawa katika utoaji wa mikopo na kutoa Elimu kwa wanufaika kwa kuzingatia aina ya Biashara na nyakati za kufanya Biashara.

‎Amewasisitiza pia juu ya uadilifu na Uwajibikaji kwa watumishi wanaowahudumia wakopaji pamoja na kuzingatia usiri huku akiwasisitiza wakopaji kurejesha kwa wakati ili wananchi wengine waweze kunufaika.



‎Awali Kaimu Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, Halmashauri ya Mji wa Bariadi, Dougias Mshana amesema Kwa mujibu wa kifungu cha 397A (1) cha Sheria ya fedha ya serikali ya mtaa sura ya 290, inaelekeza Mamlaka za Serikali za mtaa zitakuwa na wajibu wa kutenga asilimia 10 ya mapato ya ndani yasiyolindwa ya mwaka husika Kwa ajili ya vikundi vya vijana, Wanawake na Watu wenye Ulemavu.

‎"Kipindi cha robo ya tatu (January-March) kiasi cha shilingi Mil. 68.5 kilikopeshwa kwa Vikundi 7 ambapo vya vikundi vya Wanawake vilikuwa vitatu (Mil. 30.5) na vijana vilikuwa vinne (Mil. 38) na robo ya nne  vilikopeshwa vikundi 15 vyenye wanufaika 73 ambapo Wanawake vikundi 4, vijana Vikundi 9 na walemavu viwili" amesema.



‎Amesema katika kuhitimisha mwaka wa fedha 2025/26, Halmashauri ya Mji wa Bariadi imekabidhi hundi ya shilingi Mil. 222 huku akisema baadhi ya vikundi vinakosa uaminifu wa kurejesha mikopo na baadhi yao wakibadili matumizi ya fedha walizokopeshwa kulingana na miradi waliyoomba na kuanzisha miradi mipya ambayo hawana uwezo nayo.

‎Mwisho.







Post a Comment

0 Comments