DED MTIPA AWAAGIZA WACHEZAJI WA MASWA KWENDA KUTAFUTA USHINDI SHIMISEMITA.


Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Maswa, Maisha Mtipa (kushoto) akitoa maelekezo wakati akiwaaga wachezaji wa timu ya halmashauri ya wilaya ya Maswa wanaoekekea jijiniMbeya kwa ajili ya mashindano ya Shimisemita. Picha na Samwel Mwanga.

Na Samwel Mwanga,Maswa.

MKURUGENZI  Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu, Maisha Mtipa, amewaagiza wachezaji wa halmashauri hiyo watakaoshiriki Mashindano ya Shirikisho la Michezo Serikali za Mitaa( SHIMISEMITA) jijini Mbeya kuzingatia nidhamu na kupambana kuhakikisha wanarejea na ushindi.

Mtipa alitoa kauli hiyo leo, Agosti 13, 2026, katika Hoteli ya Forest mjini Maswa wakati akiwaaga wachezaji hao baada ya kuwaandalia chakula cha pamoja kabla ya safari yao kuelekea Mbeya.

Aliwataka wachezaji hao kuwa mabalozi wazuri wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa na Mkoa wa Simiyu kwa ujumla, akisisitiza umuhimu wa kuonyesha nidhamu ndani na nje ya uwanja.

Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Maisha Mtipa akizungumza wakati akiwaaga wachezaji ambao ni watumishi wa halmashauri hiyo (hawapo pichani) wanaokwenda jijini Mbeya kushiriki mashindano ya Shimisemita.Picha na Samwel Mwanga

“Michezo kwa sasa si burudani pekee, bali imekuwa sehemu ya ajira na inaunganisha watu. Hivyo, pamoja na kuwa ninyi ni watumishi wa umma, michezo pia ni sehemu ya kazi yenu na ni muhimu kuonyesha vipaji na uwezo wenu,” amesema.

Kwa upande wake, Mkuu wa msafara huo ambaye pia ni Afisa Utamaduni na Michezo wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Said Mshana, amesema timu hiyo imejiandaa vyema kwa ajili ya mashindano hayo.

Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Maswa, Maisha Mtipa (kushoto) akimuaga mmoja ya wachezaji wa timu ya halmashauri ya wilaya ya Maswa wanaoekekea jijiniMbeya kwa ajili ya mashindano ya Shimisemita. Picha na  Samwel Mwanga.

Mshana amesema wachezaji hao waliweka kambi na kucheza michezo kadhaa ya kirafiki kwa lengo la kupima uwezo wao na kubaini maeneo yanayohitaji maboresho kabla ya kuanza kwa mashindano.

Amesema wanatarajia kufanya vizuri katika michezo mbalimbali watakayoshiriki, ambayo ni pamoja na mpira wa miguu, mpira wa pete, mpira wa mikono na draft.

Mshana pia alimshukuru Mtipa kwa kuwezesha timu hiyo kuanzia maandalizi hadi kushiriki mashindano hayo, akisema msaada huo umechangia kuwaweka wachezaji katika hali nzuri ya kujiandaa na mashindano.

Jumla ya wachezaji 35 pamoja na viongozi watatu wameondoka leo kwa njia ya barabara kuelekea jijini Mbeya kuwakilisha Halmashauri ya Wilaya ya Maswa katika Mashindano ya Shimisemita 2026.

Mashindano hayo yatafanyika Agosti 15 hadi 29,2026.

Mwisho.

Gari ambayo inatumika kuwasafirisha wachezaji wa halmashauri ya wilaya ya Maswa katika mashindano ya Shimisemita huko jijini Mbeya.Picha na Samwel Mwanga.




Post a Comment

0 Comments