"BAADA YA MAONYESHO YA NANENANE, NINI HUBADILIKA MASHAMBANI?"


Mkuu wa mkoa wa Simiyu,Anamringi Macha(mwenye kofia)akiangalia vipando vya mazao mbalimbali katika viwanja wa maonesho ya nanenane vya Nyakabindi mjini Bariadi.

-Uchunguzi wa matokeo halisi ya maonesho kwa wakulima wa Simiyu.

Na Samwel Mwanga, Bariadi.

KILA mwaka maelfu ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi humiminika katika viwanja vya Nyakabindi mkoani Simiyu kushiriki Maonesho ya Nanenane. Wengine huja kujifunza teknolojia mpya, wengine kutafuta masoko, huku taasisi za utafiti, kampuni za pembejeo na wataalamu wakitumia jukwaa hilo kutoa elimu.

Lakini maonesho yanapomalizika na mabanda kufungwa, swali linalobaki ni moja: Je, kuna mabadiliko ya kweli yanayoonekana mashambani?

Uchunguzi uliofanywa na Mwandishi wa Makala hii umebaini kuwa kwa baadhi ya wakulima wa Simiyu, Nanenane si maonesho ya kutazama mashine na mabango pekee, bali ni darasa linalobadili mtazamo wa uzalishaji. 

Vipando vya mazao mbalimbali katika viwanja vya Nyakabindi mkoani Simiyu.

Hata hivyo, kwa wengine, changamoto za mtaji, pembejeo na masoko bado zinapunguza kasi ya kutafsiri elimu hiyo kuwa matokeo.

Mkulima wa pamba kutoka kijiji cha Mwabujiku,Wilaya ya Maswa,Antony Masunga anasema mara ya kwanza alipotembelea maonesho aligundua kuwa alikuwa akitumia mbegu zisizo na tija na kilimo kusichofuata kanuni bora za kilimo cha zao hilo.

"Nilikuwa nalima kama nilivyozoea kwa miaka mingi. Baada ya kupata elimu Nanenane nilianza kutumia mbegu bora na kufuata ushauri wa wataalamu. Msimu uliofuata niliona tofauti katika mavuno na ubora wa pamba."amesema. 

Zao la pamba.

Kwa mkulima wa alizeti kutoka kijiji cha Nanga,wilaya ya Itilima, Mwashi Bundala amesema maonesho yameongeza uelewa wa kuzalisha kwa kuzingatia mahitaji ya soko.

"Sasa najua si kila zao lina soko la uhakika kila wakati. Tunafundishwa kufuatilia taarifa za masoko kabla ya kuwekeza. Hilo limenisaidia kupanga uzalishaji wangu vizuri."amesema.

Wataalamu wa ugani wanasema lengo la Nanenane si kuonyesha teknolojia pekee, bali kuhakikisha maarifa hayo yanafika mashambani.

Mtaalamu mmoja wa kilimo kutoka wilaya ya Maswa, Mabula Gimu anaeleza kuwa mkulima wa sasa anatakiwa kulima kama mwekezaji.

"Kilimo cha kisasa kinaanza kwa kujua soko, kuchagua mbegu sahihi, kutumia teknolojia na kupanga uzalishaji. Hapo ndipo tija na faida vinapatikana."amesema.

Anasema matumizi ya mbegu bora, kilimo cha umwagiliaji, huduma za ugani na taarifa za masoko ni nguzo muhimu za kuongeza ushindani wa mazao ya Tanzania.

Hata hivyo, wataalamu wanakiri kuwa elimu pekee haitoshi ikiwa wakulima hawatawezeshwa kuipatia mitaji, pembejeo bora na masoko ya uhakika.

Jilingisila Mahona ni mkulima wa wilaya ya Bariadi anasema kuwa wakulima bado wanakabiliwa na changamoto za gharama kubwa za pembejeo, athari za mabadiliko ya tabianchi na upatikanaji wa wanunuzi wanaolipa bei yenye tija.

Mchambuzi wa masuala ya kilimo, Festo Michael anasema mafanikio ya Nanenane yanapaswa kupimwa kwa kile kinachotokea baada ya maonesho.

"Mafanikio si idadi ya watu waliotembelea mabanda, bali ni wakulima wangapi walibadili mbinu za uzalishaji, wakaongeza mavuno, wakaongeza thamani ya mazao na wakaongeza kipato."amesema.

Kwa mtazamo huo, Nanenane inabaki kuwa zaidi ya maonesho. Ni darasa, jukwaa la ubunifu na sehemu ya kuunganisha maarifa na fursa za biashara. 

Hata hivyo, ili matokeo chanya yaonekane kwa kiwango kikubwa zaidi, elimu inayotolewa lazima iende sambamba na uwekezaji katika huduma za ugani, upatikanaji wa mitaji, teknolojia na masoko.

Iwapo hilo litafanikiwa, wakulima wa Simiyu hawataondoka Nyakabindi wakiwa na vipeperushi na katalogi pekee, bali watarudi mashambani na mbinu mpya zitakazoongeza uzalishaji, kipato na mchango wa sekta ya kilimo katika uchumi wa Taifa.

Mwisho.






Post a Comment

0 Comments