Mbunge wa jimbo la Maswa Mashariki,Dkt George Lugomela akihutubia moja ya mikutano katika jimbo lake. Picha na Samwel Mwanga.
Na Samwel Mwanga, Maswa
WANANCHI wa Jimbo la Maswa Mashariki mkoani Simiyu wamempongeza Mbunge wao, Dkt. George Venance Lugomela, kwa kuanza ziara ya kuwashukuru baada ya kuchaguliwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, huku wakieleza kuwa hatua hiyo imewapa fursa ya kuwasilisha changamoto zinazowakabili na kupata majibu ya awali kutoka kwa viongozi na wataalamu wa Serikali.
Ziara hiyo, ambayo imeambatana na wataalamu kutoka Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, inalenga kuimarisha mawasiliano kati ya viongozi na wananchi, kusikiliza kero na kufuatilia utekelezaji wa ahadi za maendeleo zilizotolewa wakati wa kampeni.
Sehemu ya wananchi wa Kata ya Mpindo waliohudhuria mkutano wa hadhara wa mbunge wa jimbo la Maswa Mashariki, Dkt George Lugomela.Picha na Samwel Mwanga.Hadi sasa Dkt. Lugomela ametembelea kata za Mbaragane, Lalago, Dakama, Sangamwalugesha, Nguliguli, Ipililo na Mpindo, ambako amefanya mikutano ya hadhara na kusikiliza maoni ya wananchi.
Katika mikutano hiyo, wananchi wameeleza changamoto zinazohusu upatikanaji wa huduma za maji, afya, elimu, kilimo, miundombinu ya barabara, umeme na migogoro ya ardhi, huku wataalamu wakitoa ufafanuzi wa masuala yaliyohitaji majibu ya papo kwa papo na mengine yakipangwa kufanyiwa kazi.
Akizungumza na wananchi kwa nyakati tofauti tofauti Dkt. Lugomela alisema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kutekeleza miradi ya maendeleo nchini na kwamba ahadi zote zilizotolewa kwa wananchi pamoja na zilizoainishwa katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2025–2030 zitatekelezwa kwa kuzingatia mipango na uwezo wa Serikali.
Baadhi ya viongozi ambao walihudhuria mkutano wa mbunge wa jimbo la Maswa Mashariki,Dkt George Lugomela.Picha na Samwel Mwanga."Tupeni muda tuwatumikie wananchi. Ndiyo kwanza kazi tumeanza baada ya uchaguzi. Nawahakikishia wananchi wa Maswa Mashariki kuwa yale yote tuliyoahidi na yaliyomo kwenye Ilani ya CCM tutayasimamia ili yatekelezwe. Maendeleo ni hatua kwa hatua na yanahitaji ushirikiano wa wananchi wote," alisema Dkt. Lugomela.
Aliwataka wananchi kuendelea kudumisha amani, umoja na mshikamano, akieleza kuwa mazingira hayo ni msingi wa kuharakisha maendeleo ya jimbo hilo.
Baadhi ya wananchi waliozungumza na juu ya ziara hiyo walisema ujio wa mbunge huyo umeongeza imani kwa wananchi kwa kuwa umewapa nafasi ya kueleza changamoto zao ana kwa ana badala ya kusubiri kufika ofisini.
"Tumefurahi kuona mbunge ameamua kuja kutusikiliza. Hii inaonyesha anathamini maoni ya wananchi. Tunaamini changamoto tulizowasilisha zitafanyiwa kazi kwa kushirikiana na Serikali," alisema Sudi Hassan mkazi wa Kata ya Lalago.
Mkazi mwingine wa Kata ya Nguliguli,Joseph Peter alisema ziara hiyo imeonyesha dhamira ya mbunge kufuatilia maendeleo ya kila kata na kusikiliza wananchi bila ubaguzi.
"Tunamuomba asiwe na wasiwasi kutokana na maneno ya wachache. Uchaguzi ulikwisha na viongozi walishapatikana. Kilichobaki sasa ni kushirikiana kuwaletea wananchi maendeleo," alisema.
Wananchi wengine walilitaka Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuendelea kuimarisha umoja miongoni mwa wanachama wake na kuhakikisha tofauti zozote za kisiasa hazikwamishi utekelezaji wa shughuli za maendeleo katika jimbo hilo.
"Tunataka nguvu zielekezwe katika kutatua changamoto za wananchi. Siasa za uchaguzi zimeshapita, sasa ni wakati wa kufanya kazi na kuijenga Maswa Mashariki," alisema Sophia Kija.
Mbali na kueleza changamoto zao, wananchi pia waliipongeza Serikali kwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, hususan katika sekta za elimu na afya, wakisema imeongeza upatikanaji wa huduma za kijamii katika maeneo mengi ya jimbo hilo.
Vilevile waliipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Maswa kwa usimamizi wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo, wakieleza kuwa kasi ya utekelezaji inaendelea kuleta matokeo chanya kwa wananchi.
Mwisho.







0 Comments