TANZANIA YAIOMBA BENKI YA DUNIA KUIMARISHA USHIRIKIANO SEKTA YA MAJI NA MAZINGIRA.

Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Mathew ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Bariadi mjini.

Na Mwandishi wetu, Chad.

SERIKALI ya Tanzania imeiomba Benki ya Dunia, kuendelea kuimarisha ushirikiano katika Sekta ya Maji na Mazingira, ili kuongeza upatikanaji wa huduma kwa wananchi, hususani maeneo ya Vijijini.

Ombi hilo limetolewa na Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo  Mathew, alipozungumza kwa niaba ya Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, katika Kikao cha pande mbili na viongozi waandamizi wa Benki ya Dunia, kilichoketi  jijini N’Djamena, nchini Chad, tarehe 16 Julai, 2026.

Katika kikao hicho, Tanzania imeishukuru Benki ya Dunia kwa mchango wake mkubwa katika kufadhili miradi ya maji, usafi wa mazingira na kilimo na kuongeza:

"Ushirikiano wa Tanzania na Benki ya Dunia umekuwa wa mfano katika kuimarisha maendeleo ya wananchi wetu," amesema Waziri Kundo ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Bariadi Mjini, mkoani Simiyuna kuongeza.

"Tunaye Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan, ni kiongozi kinara wa Sekta ya Maji. Ameongeza Bajeti Sekta ya Maji kufikia hadi Sh Trilioni 1.12, katika mwaka wa Fedha 2026/2027," amefafanua Mhandisi Kundo. 

Kwa mujibu wa Waziri Kundo, Tanzania inaendelea kufanya mapinduzi katika huduma ya maji, hivyo ushirikiano wa Benki ya Dunia katika ufadhili wa Mpango wa Rural WASH, kupitia Program for Results (PforR), ambapo awamu ya pili yenye thamani ya Dola Milioni 200, ilianza mwaka 2025.

Amesema mpango huo unatarajiwa kukamilika mwaka 2030, baada ya awamu ya kwanza ya Dola Milioni 650 kufanikisha kuanzishwa kwa RUWASA na kuongeza upatikanaji wa  huduma ya maji maeneo ya pembezoni.

Katika kikao hicho, Tanzania imeishukuru Benki hiyo ya Dunia kwa msaada wake wa utekelezaji wa Mradi wa Pili Sekta ya Maji (WSSP II) wenye thamani ya Dola Milioni 222.8, ambao umewezesha zaidi ya watu 700,000 kupata huduma za maji, pamoja na kuboresha miundombinu ya usafi wa mazingira na huduma za maji katika maeneo mbalimbali, ikiwamo Dar es Salaam na Bagamoyo.

Katika kuhitimisha kikao hicho, Tanzania imeiomba Benki ya Dunia kuendelea kutoa msaada wa kifedha na kiufundi ili kufikisha huduma za Maji katika vijiji 1,575 ambavyo bado havijafikiwa na miundombinu rasmi ya upatikanaji wa maji pamoja na kusaidia utekelezaji wa mkubwa na wa kimkakati wa Gridi ya Taifa ya Maji (National Water Grid) sambamba na kuimarisha miradi ya usafi wa mazingira, kuongeza ushiriki wa sekta binafsi na kujenga uwezo wa taasisi za maji Nchini.

Mwisho.


Post a Comment

0 Comments