Afisa Ushirika, Mbaraka Maleu kutoka Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC)akizungumza na wakulima katika chama cha msingi cha ushirika cha Sola wilayani Maswa.
Na Samwel Mwanga, Maswa.
WAKULIMA wa zao la pamba katika Wilaya ya Maswa, mkoani Simiyu, wamepewa elimu ya namna ya kupokea malipo ya mauzo ya pamba kupitia benki na huduma za fedha kwa njia ya simu, hatua inayolenga kuongeza uwazi, usalama wa fedha na kuondoa ucheleweshaji wa malipo.
Elimu hiyo imetolewa na Maafisa Ushirika wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC) ikiwa ni maandalizi ya msimu wa ununuzi wa pamba wa mwaka 2026/2027.
Akizungumza na wakulima mjini Maswa, Aron Mrema ambaye ni Afisa Ushirika kutoka Tume ya Maendekeo ya Ushirika amesema mfumo wa malipo kupitia taasisi za fedha utasaidia wakulima kupata fedha zao kwa wakati, kupunguza hatari ya kupoteza fedha na kuongeza uwazi katika mnyororo mzima wa biashara ya pamba.
Afisa Ushirika,Aron Mrema kutoka Tume ya Maendeleo ya Ushirika(TCDC)akizungumza na wakulima katika chama cha msingi cha ushirika cha Sola wilayani Maswa.Aliwataka wakulima kuhakikisha wanafungua akaunti za benki au kusajili huduma za fedha kwa njia ya simu pamoja na kuhakiki taarifa zao kupitia AMCOS zao ili kuepusha changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa malipo.
"Serikali imeendelea kuhimiza matumizi ya mifumo ya kidijitali katika malipo ya mazao ya kimkakati, ikiwemo pamba, ili kuongeza uwazi, usalama wa fedha na kuwajumuisha wakulima katika huduma rasmi za kifedha,"amesema
Baadhi ya wakulima wa Chama cha Msingi cha Ushirika cha Sola (AMCOS) wameeleza kufurahishwa na elimu hiyo wakisema itawasaidia kuelewa mfumo mpya wa malipo.
Baadhi ya wakulima wakipata elimu juu ya malipo yao ya mazao kupitia katika taasisi za fedha iliyotolewa na Tume ya Maendeleo ya Ushirika(TCDC).Mkulima Joseph Bundala amesema hapo awali baadhi ya wakulima walikuwa hawana uelewa wa kutosha kuhusu namna fedha zinavyowasilishwa kupitia benki, hali iliyokuwa ikisababisha wasiwasi wanapocheleweshewa malipo.
"Elimu hii imetufungua macho. Sasa tunafahamu umuhimu wa kuwa na akaunti ya benki au huduma ya fedha kwa simu ili malipo yetu yafike kwa usalama na kwa wakati," amesema.
Naye Njile Emanuel amrsema mfumo huo utawasaidia wakulima kupanga matumizi ya mapato yao na kupunguza hatari ya kubeba fedha taslimu baada ya kuuza pamba.
"Tunaiomba serikali na viongozi wa ushirika waendelee kutuelimisha mara kwa mara ili kila mkulima auelewe vizuri mfumo huu na asiwe nyuma ya mabadiliko ya teknolojia," amesema.
Kwa upande wake, Jimoga Masanja amesema matumizi ya taasisi za fedha yataongeza imani ya wakulima katika mfumo wa ununuzi wa pamba kwa kuwa yataweka kumbukumbu sahihi za malipo.
"Tunatarajia msimu huu malipo yatafanyika kwa haraka zaidi kuliko ilivyokuwa zamani. Hilo litatupa hamasa ya kuongeza uzalishaji wa pamba," amesema.
Mwisho.




0 Comments