Samwel Mwanga, Bariadi.
WAKAZI wa mitaa ya Salunda na Viwandani katika Halmashauri ya mji wa Bariadi mkoani Simiyu wataondokana na adha ya upatikanaji wa maji safi na salama mara baada ya kukamilika kwa Mradi wa Maji unaotelezwa kwa gharama ya Shilingi Mil. 370.9.
Mradi huo ambao unatekelezwa na Mamlaka ya maji na Usafi wa Mazingira mjini Bariadi (Baruwasa), ulikuwa kivutio kwa kiongozi wa mbio za mwenge wa Uhuru Kitaifa, Wazo Mwang'onda ambapo amesema kuwa taarifa za Mradi huo zimeonyesha uwazi kwenye utekelezaji wake na kwamba umelenga kunufaisha wananchi 7,334.
Awali akitoa taarifa ya mradi huo leo, Julai 29, 2026, Mkurugenzi Mtendaji wa Baruwasa, Mhandisi Nandi Mathias amesema kuwa mradi huo umeanza kutekelezwa Mei 13,2026 na unategemea kumalizika Novemba 12, 2026.
Akitaja manufaa ya mradi huu, Mhandisi Nandi amesema kuwa utaimarisha uchumi wa jamii kwa kuondoa muda wa kutafuta maji safi na salama ambao watautumia katika shughuli za uzalishaji, kumtuwa mama ndoo kichwani kwa kumuondolea adha ya kutembea umbali mrefu kutafuta huduma hiyo.
"Mara baada ya kukamilika kwa mradi huu pia muda wa upatikanaji wa maji katika mitaa ya Salunda na Viwandani utaongezeka kutoka wastani wa siku mbili hadi siku saba kwa juma,"
"Huu mradi pia utaboresha afya na usafi wa mazingira wa huduma ya maji kwa taasisi za serikali ambazo ni shule ya sekondari Salunda na shule ya msingi Salunda ambazo hazikuwa na huduma ya maji,"amesema.
Amesema hadi sasa mradi huo umefikia asilimia 58 na kazi zilizofanyika katika kutekeleza mradi huo ni pamoja na ujenzi wa tenki la kuhifadhi maji lenye ujazo wa lita 50,000 katika mnara wa mita sita,mtandao wa usambazaji wa maji wenye jumla ya urefu wa Kilomita 3.38 na uchimbaji wa kisima kimoja kirefu ambacho ndicho chanzo cha maji cha mradi huo.
Kiongozi wa Mwenge wa Uhuru kitaifa,Wazo Mwang'onda akizungumza na wananchi baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa mradi wa maji wa Salunda mjini Bariadi mkoani Simiyu. Picha na Samwel Mwanga.Mkuu wa wilaya ya Bariadi, Saimon Simalenga amesema kuwa atahakikisha anausimamia mradi huo na kuhakikisha unakamilika kwa wakati ili wananchi waweze kunufaika nao.
"Mradi huu ukikamilika utaongeza hali ya upatikanaji wa maji katika mji wa Bariadi kutoka asilimia 72 hadi aslimia76,"amesema.
Baada ya kusikiliza taarifa hiyo, Mwang'onda amesema kuwa serikali inaendelea kuwasogezea wananchi huduma ya maji ili waweze kupata huduma ya majisafi na salama kwa ajili ya ustawi wa afya za wananchi.
"Baada ya muda si mrefu wananchi wa maeneo haya watapata huduma safi na salama hivyo niwaombe mdumishe amani na utulivu sambamba na kutunza hii miundombinu ya maji iliyoko kwenye mradi huu,"amesema.
Kiongozi wa Mwenge wa Uhuru kitaifa, Wazo Mwang'onda akizungumza na wananchi baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa mradi wa maji wa Salunda mjini Bariadi mkoani Simiyu.Picha na Samwel Mwanga.Magawa Itilinga ni mkazi wa mtaa wa Salunda amesema kuwa mradi huo utakapokamilika utawasaidia kupunguza umbali wa kutembea muda mrefu kutafuta maji safi na salama.
"Maji tunayapata kwa umbali wa kilomita 10 hivyo tunatumia muda mrefu kufuata maji ambayo yanapatikana kwenye kisima hivyo tunaomba kasi iongezwe kwa ajili ya kukamilisha mradi huu,"amesema.
Naye Mariam Malimi mkazi wa mtaa wa Viwandani amesema kuwa maji wanayotumia kwa sasa si safi na salama kwani yanapatikana kwenye mto hivyo serikali ihakikishe inausimamia mradi huo kwa nguvu zote,"amesema.
Kwa upande wake,Bulude Mishono mkazi wa mtaa wa Viwandani amesema kuwa wanawake wa maeneo hayo wamekuwa wakitumia muda mrefu kutafuta maji kutokana na eneo hilo kutokuwa na huduma ya upatikanaji wa maji na wakati mwingine baadhi ya familia kutoelewana kutokana na wakinamama kutumia muda mrefu kufuata maji.
"Kuna baadhi ya wanawake wamekuwa wakigombana na wanaume zao kwa kile kinachodaiwa kuwa wamekuwa wakitumia muda mrefu kutafuta maji lakini baadhi ya wanaume wanasema kuwa walikuwa kwenye masuala mengine na si maji," Amesema
Mwisho.
Mkurugenzi Mtendaji wa Baruwasa,Mhandisi,Nandi Mathias akitoa taarifa ya ujenzi wa mradi wa maji wa Salunda mjini Bariadi kwa kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru Kitaifa,Wazo Mwang'onda (hayupo pichani).Picha na Samwel Mwanga.



0 Comments