Na Samwel Mwanga.
HALMASHAURI ya Wilaya ya Maswa imeanza mafunzo ya siku tatu ya uenezaji wa Mwongozo wa Chakula na Ulaji – Kitabu cha Jamii (Tanzania Bara), hatua inayolenga kuimarisha mapambano dhidi ya utapiamlo na kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu lishe bora.
Mafunzo hayo, yaliyoanza Julai 23, 2026 katika Ukumbi wa Hoteli ya Kaisi mjini Maswa, yamewakutanisha Maafisa Lishe wa halmashauri, walimu wa afya na lishe kutoka shule za msingi na sekondari, waratibu wa watoa huduma za afya ngazi ya jamii pamoja na maafisa kutoka idara mbalimbali za wilaya.
Akifungua mafunzo hayo, wataalamu walieleza kuwa lengo ni kuwajengea washiriki uwezo wa kufikisha elimu sahihi ya lishe kwa jamii ili kuboresha afya, kupunguza utapiamlo na kukabiliana na ongezeko la magonjwa yasiyoambukizwa yanayohusishwa na ulaji usiofaa.
Katika siku ya kwanza ya mafunzo, washiriki walipata utangulizi kuhusu shirika la Nutrition International (NI) na utekelezaji wa mradi wa REACTS-IN (Realizing Gender Equality, Attitudinal Change and Transformative Systems in Nutrition), uliowasilishwa na Afisa Mwandamizi wa Nutrition International, Laureta Lucas.
Washiriki pia walipewa taarifa kuhusu matokeo ya uchambuzi wa usawa wa kijinsia unaotekelezwa katika wilaya za Maswa na Meatu, ukionesha umuhimu wa kuwawezesha wanawake na wasichana katika kuboresha lishe ya familia na afya ya watoto.
Kwa mujibu wa wataalamu, mradi wa REACTS-IN unatekelezwa nchini Tanzania kuanzia mwaka 2023 hadi 2030 ukiwa na lengo la kuboresha afya na lishe ya wanawake, wasichana balehe na watoto wenye umri chini ya miaka mitano kupitia afua zinazozingatia usawa wa kijinsia. Kimataifa, mradi huo unatarajiwa kuwafikia zaidi ya wanufaika milioni 1.3 katika nchi nne.
Aidha, wataalamu kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), wakiongozwa na Afisa Lishe Mtafiti Mwandamizi, Maria Ngilisho, walitoa mafunzo kuhusu Mwongozo wa Chakula na Ulaji kwa Tanzania Bara na mchakato wa kuandaa mwongozo huo ili kuhakikisha wananchi wanapata elimu ya lishe inayozingatia mazingira, tamaduni na vyakula vinavyopatikana nchini.
Katika mafunzo hayo, washiriki walisisitizwa umuhimu wa kula mlo kamili unaojumuisha makundi sita ya vyakula kila siku, ambayo ni nafaka, mizizi na ndizi; mikunde, karanga na mbegu; vyakula vya asili ya wanyama; mafuta yenye afya; mboga mboga; na matunda.
Wataalamu walieleza kuwa matumizi ya vyakula vya aina mbalimbali kutoka katika makundi hayo husaidia mwili kupata virutubishi muhimu vinavyochangia ukuaji wa watoto, kuimarisha kinga ya mwili, kuongeza uwezo wa kujifunza na kufanya kazi, pamoja na kupunguza hatari ya utapiamlo na magonjwa yasiyoambukizwa, yakiwemo kisukari, shinikizo la damu na magonjwa ya moyo.
Kupitia mafunzo hayo, Halmashauri ya Wilaya ya Maswa inalenga kuwawezesha wataalamu na wadau wa afya kuendelea kueneza elimu sahihi ya lishe katika ngazi ya jamii, hatua inayotarajiwa kuchangia kujenga jamii yenye afya bora, nguvu kazi yenye tija na kizazi chenye maendeleo endelevu.
MWISHO




0 Comments