MANUSURA WA KULIWA NA MAMBA, AMWOMBA RAIS DK. SAMIA NA WATANZANIA KUMSAIDIA.

 

YOEL Edward (32), Manusura wa Kuliwa na Mamba akiwa amekaa kwenye kiti mwendo, akionyesha sehemu ya miguu yake iliyowekewa vyuma kutokana na kushambulia na Mamba. (Tunaomba radhi Kwa picha hizo).

Na COSTANTINE MATHIAS.

KILA anapotazama miguu yake iliyojaa vidonda, mifupa iliyo wazi na vyuma vilivyowekwa kwa ajili ya kuokoa maisha yake, Yoel Edward (32) anakumbushwa tukio la kunusurika kuliwa na Mamba ambalo lilibadili maisha yake milele. 

Ndoto za kijana huyu wa kujitegemea kupitia kilimo zilivunjika ndani ya sekunde chache baada ya kushambuliwa na mamba katika Mto Kisaki, uliopo Kijiji cha Migolegole, Kata ya Mgazi, Wilaya ya Morogoro Mkoani Morogoro.

Leo, zaidi ya mwaka mmoja tangu tukio hilo litokee kwa kijana Yoel ambaye anaishi kwa maumivu makali kila siku iendayo kwa Mwenyezi Mungu.

Hawezi kutembea, hawezi kufanya kazi na hawezi kumudu gharama za matibabu, lakini anasema matumaini yake makubwa sasa ni msaada kutoka kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Serikali na Watanzania wenye moyo wa huruma kumpatia Msaada ili aweze kupata matibabu na kuanza maisha mapya.

Safari ya kutafuta maisha iliyogeuka mateso

Yoel anasimulia kuwa awali Familia yao walikuwa wanaishi Sengerema Mkoani Mwanza, baada ya baba yake kufariki dunia, familia ililazimika kuhama na kwenda Morogoro kutafuta maisha kupitia shughuli za kilimo.

"Baada ya baba kufariki tulihamia Morogoro kwa ajili ya kilimo, huko ndipo nilianza kufanya kazi za shambani kwa kulima mpunga na Ufuta ili kusaidia familia kwa sababu mimi ndie kijana Mkubwa," anasema.

Kwa muda maisha yaliendelea vizuri hadi ilipofika Machi 17, 2025, siku ambayo hataisahau maishani mwake kwani siku hiyo alikwenda kuangalia sehemu ya kuchota maji kwa ajili ya umwagiliaji wa mazao.

Anasema kwamba baada ya kuchota maji alisimama pembeni ya mto akisafisha miguu bila kujua kuwa hatari ya kuliwa na Mamba ilikuwa imemkaribia.

"Ghafla nilihisi nimerushwa ndani ya mto. Sikuelewa kilichotokea mpaka nilipogundua miguu yangu imeshikwa na mamba." Anasema Yoel.

Mamba huyo alianza kumvuta kwa nguvu ndani ya maji huku akimpeleka kwenye matete yaliyokuwa pembezoni mwa mto.

"Maji hayakuwa mengi sana, lakini nguvu zake zilikuwa kubwa. Nilihisi ndiyo mwisho wa maisha yangu." Anasimulia mbele ya waandishi wa Habari huku akibubujikwa machozi.

Anafafanua kuwa baada ya muda, mamba alimwachia na hakujua ni kwa nini aliachiwa, lakini alitumia nguvu zake zote kujivuta hadi ukingoni mwa mto.

"Nilipofika ukingoni ndipo nilipoona ukubwa wa majeraha. Miguu ilikuwa imeharibika vibaya, baadhi ya mifupa na nyama zilikuwa zimekatika kabisa." Anasema.

Kilio kilichookoa maisha yake

Akiwa katika maumivu makali, Yoel alianza kupiga kelele kuomba msaada na kwa bahati nzuri wachungaji waliokuwa karibu waliinusuru maisha yake baada ya kusikia sauti yake.

"Walikuja waliponikuta wamekuta nimekaa pembeni ya mto nikiwa siwezi kusimama...walinibeba na kuniweka kivulini." Anasema Manusura huyo.

Baadaye alipelekwa Kituo cha Afya Kisaki ambako alipatiwa huduma za kwanza na kuandikiwa PF3 kabla ya kuhamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro.

Hospitali hiyo ilifanya mawasiliano na TANAPA ili kuhakikisha anapatiwa matibabu ya haraka.

"Sikumbuki mengi kwa sababu nilikuwa nimezimia kutokana na maumivu makali na kupoteza damu nyingi."

Anaeeleza kuwa alipokuja kupata fahamu alijikuta tayari amelazwa hospitalini huku miguu ikiwa imefungwa vyuma vya kusaidia mifupa.

Safari ya Muhimbili.

Baada ya mwezi mmoja kuisha akiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, madaktari waliona majeraha yalihitaji matibabu ya kibingwa.

Yoel alipewa rufaa kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo (MOI) kwa ajili ya huduma na uangalizi zaidi.

"Nilikaa Muhimbili karibu miezi miwili, vidonda vilikuwa vimechafuka sana na vilianza kuoza kwani baadhi ya mifupa na nyama zilisalia mtoni" anasema.

Anasema kwamba Madaktari walianza kushughulikia, kuliko mguu wa kushoto.

"Waliniambia nyama nyingi zilikuwa zimepotea pamoja na kipande cha mfupa. Walipandikiza sementi ya mfupa pamoja na nyama."

Baada ya matibabu hayo, alipewa ruhusa ya kurudi nyumbani kwa ajili ya kuendelea na uangalizi, lakini mambo hayakwenda kama ilivyotarajiwa kutokana na kwamba ngozi iliyokuwa imeshonwa iliteleza, ikaoza na kutengeneza shimo kuwa na kile kipande kilichowekwa ndani hakikushika.

Matibabu yanasimama kwa kukosa fedha.

Anasema tangu alipotoka Muhimbili mwezi Juni mwaka jana hajawahi kurejea tena kwa matibabu kutokana na hali ngumu ya kifedha.

Badala yake, familia ilihamia Yoma, Kata ya Somanda, Halmashauri ya Mji wa Bariadi kwa ndugu wakitarajia kupata msaada.

"Hadi leo sijapata matibabu yoyote sababu changamoto kubwa ni fedha. Nawaomba Watanzania wenzangu wanisaidie ili niondokane na adha ya maumivu ninayopata kila siku" anasema.

Maumivu yasiyoisha.

Kadiri siku zinavyopita, hali yake inazidi kuwa mbaya, Vidonda vinaendelea kutoa usaha huku vyuma vilivyowekwa ndani ya miguu vikisababisha maumivu makali.

"Mifupa ipo wazi, Siwezi kutembea...Najivuta kwa kutumia mikono au nakaa kwenye kiti cha magurudumu, Kila siku nalazimika kutumia dawa za maumivu ili kupunguza mateso ninayoyapitia." Anasema.

Anaongeza kuwa, Madaktari walimweleza kuwa mguu wa kushoto umeharibika zaidi, huku wakishauri mguu wa kulia ukatwe ili kuongeza nafasi ya kuokoa maisha yake.

Kwa Yoel, huo ni uamuzi mgumu, lakini anasema iwapo ndiyo njia pekee ya kuendelea kuishi, yuko tayari.

Gharama kubwa zinazozuia matibabu.

Changamoto kubwa kwa sasa inayomkabili kijana huyo ni ukosefu wa fedha na anasema operesheni ya mguu mmoja pekee inahitaji takribani shilingi 800,000, fedha ambazo familia yake haina uwezo wa kuzipata.

Zaidi ya hapo, bado zinahitajika fedha za dawa, vipimo, viungo bandia endapo mguu utakatwa, usafiri na gharama nyingine za hospitali.

"Nawaomba Watanzania wanisaidie, naomba Serikali na viongozi wake waniangalie Kwa jicho la huruma sababu nateseka".

Ombi kwa Rais Dkt. Samia.

Kwa sauti ya unyenyekevu, Yoel anamwomba Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuingilia kati ili aweze kupata matibabu.

"Namuomba Rais Dkt. Samia anisaidie nipate matibabu, viungo bandia pamoja na mtaji wa kuanza maisha mapya."

Anasema hata kama atapona, hawezi tena kufanya kazi nzito za kilimo kama alivyokuwa akifanya zamani.

"Nahitaji mtaji wa kuanzisha biashara ndogo ili niweze kujitegemea."

Mama auza kila kitu.

Mama mzazi wa Yoel, Felister Magembe, anasema maisha ya familia yalibadilika kabisa baada ya mtoto wake kujeruhiwa.

"Nimeuza nyumba, mashamba, viwanja na mali nyingine zote nilizokuwa nazo ili kumtibu mwanangu."

Anasema kwa sasa wanaishi kwa msaada wa ndugu huku wakifanya vibarua vidogo ili kupata fedha za kununua dawa za maumivu.

"Kila nilichokuwa nacho kimekwisha. Sasa sina uwezo hata wa kumpeleka hospitalini."

Anasema jambo analoliomba kwa Watanzania ni msaada wa matibabu na hata bima ya afya.

"Nawaomba wenye uwezo watusaidie. Hata bima ya afya itatusaidia sana."

Serikali ya mtaa yathibitisha hali hiyo.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Yoma, Kata ya Somanda, Halmashauri ya Mji wa Bariadi, Yohana Mahangila, anasema familia hiyo ilifika katika eneo hilo mwaka 2025.

Anasema baada ya kupata taarifa alitembelea familia hiyo na kujionea hali halisi ya Yoel.

"Tuliwaandikia barua kwenda kwa Mkuu wa Wilaya ili kuomba msaada wa matibabu."

Anasema bado kijana huyo anahitaji msaada wa haraka kabla hali yake haijawa mbaya zaidi.

"Ninaomba Watanzania wote watakaoguswa na simulizi hii wamchangie ili apate matibabu."

Ndoto bado ipo.

Pamoja na maumivu makali anayopitia kila siku, Yoel hajakata tamaa kwani anaamini ipo siku atarejea katika maisha ya kawaida ikiwa atapata matibabu stahiki.

Anasema lengo lake si kuendelea kutegemea misaada maisha yote, bali kupata fursa ya kusimama tena na kujitegemea.

"Nikipona natamani nipate mtaji wa biashara. Sitaki kuendelea kuwa mzigo kwa familia."

Kwa sasa, tumaini lake kubwa limebaki kwa Watanzania wenye moyo wa huruma, taasisi mbalimbali za misaada na Serikali.

Anasema msaada wowote, mkubwa au mdogo, unaweza kubadili maisha yake.

"Ninaomba msiniache. Naomba mnisaidie nipate matibabu. Nataka kuishi."

Kwa yeyote atakayeguswa na simulizi ya Yoel Edward na kutaka kumchangia kwa ajili ya matibabu na mahitaji mengine muhimu, anaweza kuwasiliana naye kupitia namba 0668 531 520.

Huenda msaada huo ukawa mwanzo wa kurejesha matumaini ya kijana ambaye maisha yake yalibadilishwa ghafla na shambulio la mamba akiwa katika harakati za kutafuta riziki.

Mwisho.




Post a Comment

0 Comments