ENG. KUNDO AGAWA SEMENTI MIFUKO 430, PAMPU ZA MAJI 17 NA MABATI 104 ISANGA, ASIKILIZA KERO ZA WANANCHI. ‎

MBUNGE wa Jimbo la Bariadi Mjini, Mhandisi Kundo Mathew (aliyeshika kipaza sauti) akikabidhi bati 104 Kwa ajili ya kukamilisha Vyumba vya madarasa Shule ya Msingi Isanga A, iliyoko Halmashauri ya Mji wa Bariadi.

‎Na COSTANTINE MATHIAS. Bariadi.

‎MBUNGE wa Jimbo la Bariadi Mjini, Mhandisi Kundo Mathew ameanza ziara ya Kata kwa Kata kwa ajili ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi, huku akitumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha za kutekeleza miradi ya Maendeleo kwenye sekta za Maji, Umeme, Barabara, na Elimu katika Jimbo lake.

‎Akizungumza leo Julai 20, 2026, katika ziara hiyo, pamoja na mambo mengine Mhandisi Kundo amekabidhi mifuko 430 ya saruji na mabati 104 ili kuboresha sekta ya Elimu pamoja na pampu za maji 17 ambazo zitafungwa kwenye visima vya Maji ili kuboresha upatikanaji wa Maji safi na salama kupitia Mpango wa dharura.

‎Mifuko 430 ya saruji iliyokabidhiwa na Mbunge wa Jimbo la Bariadi mjini, Mhandisi Kundo Mathew kwa ajili ya kutekeleza miradi ya Elimu kata ya Isanga.

‎"Shule ya Msingi Isanga A, watapokea mifuko 100 ya saruji na mabati 104, Isanga C mifuko 100, Katenga Sekondari mifuko 200 na Majahida Shule ya msingi mifuko 30...tunajenga shule mpya ya Msingi Mwatungu kwa gharama ya Shilingi Mil. 304 ili kuwaondolea wanafunzi adha ya kutembea umbali mrefu" amesema na kuongeza.

‎'Halmashauri ya Mji wa Bariadi ina mitaa 92, nimetathimini na kubaini kuna wananchi wa mjini, maisha yao yanafanana na Wananchi wa vijijini...tumechukua mitaaa 63 na kuwasilisha serikali ili wananchi waunganishiwe Umeme kwa gharama ya Shilingi elfu 27, hii ni kazi Dk. Samia."

‎

MBUNGE wa Jimbo la Bariadi Mjini, Mhandisi Kundo Mathew (wa pili kushoto) akikabidhi pampu za maji 17 kwa ajili ya visima vya Maji kata ya Isanga, Halmashauri ya Mji wa Bariadi.

‎Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira (Baruwasa), Mhandisi Nhandi Mathias amesema kuwa serikali imetoa kiasi cha shilingi Bil. 1.2 kwa ajili ya kutekeleza mradi wa Maji kata ya Isanga ambapo fedha hizo zitatumika kujenga tenki la Maji na kununua Mabomba ya Maji yatakayotandazwa urefu wa kilometa 25.

‎Amefafanua kuwa mradi huo wa muda mfupi utatekelezwa ndani ya miez sita na kwamba maeneo ya Londo na Wala watakwenda kupata Maji safi na salama a pia pampu 17 zilizokabidhiwa na Mbunge huyo zitapunguza adha ya Maji kwa wananchi wa Kata ya Isanga.


‎Awali, wananchi wa Kata ya Isanga wameiomba serikali kuboresha miundombinu ya Barabara pamoja na kufikisha Umeme Katenga Sekondari ili wanafunzi waweze kupata Elimu katika Mazingira mazuri.

‎Limi Silanga, mkazi wa Majahida ameiomba serikali kutatua migogoro ya ardhi hususani katika upimaji wa viwanja ili wananchi wamilikishwe maeneo yao ambayo yatawawezesha kupata mikopo pamoja na huduma nyinginezo muhimu.

‎Mhandisi Kundo ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maji, ameanza ziara ya hatua kwa hatua katika kata ya Isanga iliyoko Halmashauri ya Mji wa Bariadi Mkoani Simiyu ambapo aliwashukuru wananchi kwa kuendelea kuiunga Mkono serikali iliyoko madarakani.

‎Mwisho.

Post a Comment

0 Comments