NAFASI YA WAWINDAJI WA TEMBO AU BAYEGE KATIKA ARDHI YA UNYAMWEZI.



Na Augustino Manjale, Tabora.

WAWINDAJI wa Tembo katika Kabila la Wanyamwezi walifahamika kama BAYEGE au WAYEGE, naaminika kuwa BUYEGE ulikuwa kwa kasi sana mwishoni mwa Karne ya kumi na nane (1700's) na mwanzoni mwa Karne ya kumi na tisa ( 1800's) baada ya Wanyamwezi kufanikiwa kufika Pwani, katika Dola ya Mrima ambapo walikutana na Biashara ya Meno ya Tembo "Mino ga Nzovu" nulu "Mino ga Mhuli".

Basi waliporudi, Unyamwezi walianza kujikusanya makundi makundi huku wakijihusisha na shughuli za madawa na matambiko kwa ajili ya kuwinda Tembo.

Inasimuliwa kuwa Wawindaji walipokuwa njiani na Safarini kuwinda Tembo walikuwa wakiimba nyimbo na kucheza Ngoma kama njia ya kujifariji katika shughuli hiyo ya uwindaji wa tembo. 

Baadaye ilikuja kuzaliwa jumuiya ya Buyege iliyojihusisha na matambiko pamoja na madawa ya Wawindaji wa Tembo na kukubalika katika jamii mbalimbali za Wanyamwezi. 

Basi Wawindaji hawa wa Tembo walipokuwa wakiua Tembo katika utemi Fulani walitakiwa kupeleka Pembe moja ikulu kwa Mtemi na Kubakia na wao na Pembe moja. Wakiua wawili au zaidi walifanya vivyo hivyo. Hii ilikuwa kama kulipa Kodi katika utemi au nchi hiyo.

Wayege walipo ua Tembo na kupeleka Jino la Tembo walipatiwa zawadi na Mtemi. Waliweza kupewa Watumwa wawili na chupa moja ya Baruti pamoja na fataki mia au waliweza kupewa mitumba miwili ya nguo. Kwani kuua Tembo ilihesabika kama ushujaa.

NAFASI ZA BAYEGE KATIKA FALME ZA WANYAMWEZI.

Mtemi alipotakiwa kunyolewa nywele, hakunyolewa nywele kama watu wa kawaida walivyonyolewa nywele. Bali alinyolewa nywele na Bayege yaani Wawindaji wa Tembo. 

Bayege walitakiwa kuua Tembo Kisha kumchukua Mtemi na Mke wake na kwenda kuwapandisha juu ya Mgongo wa Tembo waliomuua, ndipo Mtemi alinyolewa Nywele zake. Hii ndiyo ilikuwa Mila na Desturi katika Sheria za kuwanyoa Nywele Watemi wa Wanyamwezi kabla ya Ujio wa dini na ukoloni.

Vile vile Mtemi alipofariki, Kifo chake kiliombolezwa kwa ngoma za Wawindaji wa Tembo, yaani "NGOMA ZA BUYEGE" pamoja na ngoma za Wakota au Wakango. Usiku kucha zilichezwa ngoma hizo. Wakati wa Maziko Waganga na Bayege walishughulika kufanya Buyege ndani kwa Mtemi alipo hifadhiwa. 

Lakini pia Maiti ya Mgabangoma (Mtemi aliyefariki) inapotolewa nje kuelekea malaloni (Mazimbo) Bayege walitangulia mbele kwanza ndipo Waganga yaani Bafumu wanafuata nyuma na kwenda kumzika Mtemi. Yapo mambo Mengi yanayofanyika kabla ya kumzika Mtemi, Leo nimejaribu kuzungumzia nafasi ya Wayege katika Mila na Desturi za Wanyamwezi nyakati za kale.

Hayo ni machache ninayoyafahamu kuhusu Wayege yaani Wawindaji wa Tembo ndani ya ardhi ya Unyamwezi. Uwindaji wa Tembo uliiwafanya Wanyamwezi kufika maeneo mbalimbali ya Tanzania na nje ya Tanzania katika Karne ya 18 na 19.

Makala hii imeandikwa na Mchambuzi wa Historia ya makabila ya Wanyamwezi, Wasumbwa na Wasukuma Ndugu, Augustino Manjale 0785165047/What's app 0625690038.

Mwisho.

Post a Comment

0 Comments