MBOLEA HAI YA NAVIAKOSH YAONYESHA MAFANIKIO UONGEZAJI TIJA ZAO LA PAMBA.

Na Mwandishi Wetu

WAKULIMA wa pamba katika Kijiji cha Mwamondi, Kata ya Dutwa, wameiomba serikali kuendelea kusisitiza matumizi ya mbolea hai katika kilimo cha pamba na kusema kuwa hatua hiyo itaongeza uzalishaji, kuwaongezea kipato na kuchangia kukuza uchumi wa Tanzania.

Mkulima wa pamba, Mgema Kihinda, amesema amefanya majaribio ya kutulumia mbolea ya Naviakosh katika msimu wa kilimo wa 2025/2026 na kushuhudia tofauti kubwa ya uzalishaji. 

Ameeleza kuwa shamba alilowekea mbolea lina mimea yenye afya, vitumba vingi na matarajio makubwa ya mavuno ikilinganishwa na shamba ambalo halikutumia mbolea.

Kwa upande wake, Michael Nigo amesema mazao yaliyowekewa mbolea hiyo yameonyesha ukuaji mzuri na kuwa na vitumba vingi zaidi. Alibainisha kuwa baadhi ya mimea ina vitumba kati ya 50 hadi 100, tofauti na mashamba ambayo hayakuwekewa mbolea.

Naye Minza Kichambula amesema uzalishaji katika shamba lake bado ni mdogo kutokana na kutotumia mbolea ya kutosha, hivyo akaiomba serikali na wadau wa kilimo kuwasaidia wakulima kupata elimu ya utengenezaji na matumizi ya mbolea ili kuongeza mavuno.

Kilaga Shebe amesema wakulima waliotumia mbolea ya Naviakosh wamepata matokeo mazuri, hivyo kuna umuhimu wa kuwafikia wakulima wengi zaidi kwa mafunzo yatakayowawezesha kuongeza uzalishaji wa pamba na kuboresha kipato cha kaya zao.

Afisa Kilimo wa BBT na mwezeshaji wa majaribio ya mbolea ya Naviakosh, Benjamini Benedicto, amesema wakulima wamepewa mafunzo ya kutengeneza mbolea hiyo kwa kutumia malighafi zinazopatikana kwa urahisi, ikiwemo kinyesi kikavu cha ng'ombe, unga wa dengu, molasisi, majivu na bakteria wa Naviakosh.

Amefafanua kuwa mbolea hiyo hutoa virutubisho muhimu vya Nitrogen, Phosphorus na Potassium vinavyosaidia kuimarisha rutuba ya udongo na ukuaji wa mazao, Aidha, amesema mbolea huwa tayari kwa matumizi baada ya siku 10 hadi 14 tangu kuandaliwa.

WAKULIMA wa Pamba wameiomba serikali kusisitiza matumizi ya mbolea ili kuongeza tija ya uzalishaji wa pamba kwa lengo la kuowaongeza kipato na kukuza Uchumi wa Tanzania.

‎"Mahitaji ni kinyesi cha Ng'ombe kikavu kilo 2,000 sawa na tani 2, Unga wa Dengu kilo 20,. sukari guru (molasisi) Lita 10, majivu kilo 200 na kilo moja ya Naviakosh au Bakteria wanaoenda kuzalishwa baada ya kukamilisha mbolea hiyo itakuwa na Nitrogen, Phosphorus na Potassium kwa sababu kinyesi Cha Ng'ombe, (nitrogen) Dengu (Phosphorus) na Majivu (potassium)" amesema.

Wakulima hao wameitaka serikali kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya kilimo kuendelea kuhamasisha matumizi ya mbolea na kutoa mafunzo kwa wakulima wengi zaidi, wakiamini kuwa hatua hiyo itaongeza uzalishaji wa pamba, kuboresha maisha ya wakulima na kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa.

MWISHO.


Post a Comment

0 Comments