Na Samwel Mwanga, Maswa.
MKUU wa Wilaya ya Maswa, Dk. Vincent Naano, amesema mapambano dhidi ya ugonjwa wa malaria yanapaswa kuelekezwa zaidi katika ngazi ya jamii ili kuhakikisha ugonjwa huo unatokomezwa kabisa na kufikia lengo la kuwa na jamii isiyo na malaria.
Dk. Naano amesema hayo wakati akizindua zoezi la kunyunyizia dawa ya viuatilifu vya kibaiolojia vya mbu wanaoambukiza ugonjwa wa malaria katika mabwawa, madimbwi na maeneo mengine yanayotumika kama mazalia ya mbu katika Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu.
Mkuu wa wilaya ya Maswa, Dkt Vicent Naano akizungumza kabla ya kuanza kaa zoezi la kupulizia dawa ya viuadudu vya kibailojia vya mbu wanaoneza ugonjwa wa malaria. Picha na Samwel MwangaAmesema kuwa iwapo kila mwananchi atashiriki kikamilifu katika vita dhidi ya malaria kwa kuhakikisha mazingira yanakuwa safi, kuondoa mazalia ya mbu na kutumia vyandarua wakati wa kulala, wilaya hiyo inaweza kufikia kiwango cha sifuri ya maambukizi ya malaria.
“Ikiwa kila mmoja atatimiza wajibu wake wa kutunza mazingira na kutumia chandarua, tunaweza kufikia lengo la kuwa na jamii isiyo na malaria. Vita hii haiwezi kuachiwa sekta ya afya pekee, ni jukumu la kila mwananchi,” amesema Dkt Naano.
Ametoa wito kwa watendaji wa afya kuhakikisha dawa hizo hazibaki maghalani bali zinasambazwa katika kata zote za wilaya hiyo na kutumika kunyunyizia mabwawa na madimbwi yote yanayotambulika kuwa mazalia ya mbu.
Aidha, amesisitiza kuwa hakuna mwananchi anayepaswa kutozwa fedha yoyote katika utekelezaji wa zoezi hilo kwa kuwa Serikali imegharimia dawa hizo kwa lengo la kulinda afya za wananchi.
“Serikali imegharamia dawa hizi ili kuhakikisha mazalia ya mbu yanaangamizwa. Haya ni mapambano dhidi ya ugonjwa hatari wa malaria, hivyo hakuna mwananchi anayepaswa kutozwa gharama ya aina yoyote,” amesema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Maisha Mtipa, amesema ugonjwa wa malaria umeendelea kuwa tishio kwa maisha ya wanawake wajawazito na watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano, licha ya huduma za matibabu kupatikana katika vituo vya afya vilivyopo wilayani humo.
Amesema halmashauri imeamua kuongeza nguvu katika kuangamiza mazalia ya mbu ili kupunguza maambukizi na kujenga jamii yenye afya bora.
Kwa upande wake, Mratibu wa Malaria Wilaya ya Maswa, Naomi Nyangindu, amesema kiwango cha maambukizi ya malaria wilayani humo kimepungua kutoka asilimia 21 hadi asilimia 3 kwa kipindi cha mwezi April hadi Juni mwaka huu kutokana na juhudi mbalimbali zinazofanywa na Serikali na wadau wa afya.
Amesema mafanikio hayo yametokana na utoaji wa elimu kwa wananchi, matumizi ya vyandarua vyenye dawa na kuangamiza mazalia ya mbu kwa kutumia viuatilifu vya kibaiolojia.
Nyangindu amesema wilaya hiyo imepokea lita 900 za dawa za kunyunyizia mazalia ya mbu zenye thamani ya Sh milioni 10 zilizotolewa na Serikali, na kwamba dawa hizo zitatumika katika maeneo yote yenye mabwawa na madimbwi.
Mratibu wa Malaria wilaya ya Maswa,Naomi Nyangindu(aliye kati)akisoma taarifa ya kiwango cha ugonjwa wa malaria katika wilaya ya Maswa.Picha na Samwel Mwanga.“Dawa hizi hazina madhara kwa binadamu wala wanyama. Zinaua vijidudu vya kibaiolojia vinavyosababisha kuzaliana kwa mbu wa malaria pekee, hivyo wananchi wasiwe na hofu yoyote,” amesema.
Baadhi ya wananchi wamepongeza hatua hiyo wakisema itaongeza ulinzi dhidi ya ugonjwa wa malaria na kupunguza gharama za matibabu kwa familia nyingi.
Lucy John, mkazi wa Kitongoji cha Mnadani mjini Maswa, amesema kampeni hiyo imekuja kwa wakati muafaka kwani malaria imekuwa ikisababisha usumbufu mkubwa kwa wananchi hasa wakati wa mvua.
“Tunashukuru Serikali kwa kuleta dawa hizi. Tunaamini zitasaidia kupunguza mbu na kutulinda dhidi ya malaria ambayo imekuwa ikituathiri mara kwa mara,” amesema.
Naye Lydia Mathias, mkazi wa Mjiapanda mjini Maswa, amesema wananchi wanapaswa kuendelea kutunza mazingira yao sambamba na kutumia vyandarua ili kufanikisha vita dhidi ya malaria.
“Dawa peke yake haitoshi. Sisi wananchi pia tunapaswa kuhakikisha tunafagia mazingira yetu na kuondoa maji yaliyotuama ili kuzuia mbu kuzaliana,” amesema.
Kwa upande wake, Daniel Samwel, mkazi wa Majebele mjini Maswa, amesema ushirikishwaji wa wananchi katika kampeni za afya ni muhimu kwa kuwa huongeza uelewa na kuwafanya kuwa sehemu ya suluhisho la changamoto za afya katika jamii.
“Tunapopewa elimu na kushirikishwa katika kampeni kama hizi tunakuwa na hamasa ya kushiriki. Tunaamini malaria inaweza kutokomezwa ikiwa kila mmoja atatekeleza wajibu wake,” amesema.
Zoezi la kunyunyizia viuatilifu vya kibaiolojia katika mazalia ya mbu linatarajiwa kufanyika katika kata zote za Wilaya ya Maswa kama sehemu ya mkakati wa Serikali wa kupunguza maambukizi na hatimaye kutokomeza ugonjwa wa malaria nchini.
Mwisho.
Mkurugenzi Mtendaji wa halmaahauri ya wilaya ya Maswa, Maisha Mtipa akinyunyizia dawa ya Viuadudu vya kibaiolojia vya mbu waenezao ugonjwa wa malaria katika bwawa la Mwantoja mjini Maswa.Picha na Samwel Mwanga. 




0 Comments