Mtambo wa Zimamoto na Uokoaji wilaya ya Busega uliotolewa na Serikali kuimarisha huduma za majanga na kudhibiti moto.Na COSTANTINE MATHIAS, Busega.
KAIMU Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Simiyu, Faustine Mtitu amesema kuwa Mtambo wa kuzimia Moto uliotolewa na Serikali wilayani Busega Mkoani humo una uwezo wa kuzima moto mpaka kwenye jengo la ghorofa 12.
Mtambo huo wa kisasa ambao ni gari lenye uwezo wa kupambana na ajali zote za Moto na Uokoaji, limekabidhiwa kwa viongozi wa Wilaya hiyo ili kuimarisha huduma za kukabiliana na majanga ya moto, kuokoa maisha ya wananchi na kulinda mali zao.
Akizungumza jana katika hafla ya kukabidhi mtamb huo mbele Mkuu wa Wilaya hiyo Faiza Salum, Kamanda Mtitu, amesema mtambo huo utaongeza uwezo wa jeshi hilo kutoa huduma za dharura kwa haraka na ufanisi zaidi pindi majanga yanapotokea.
Mtitu amesema kuwa mtambo huo unao uwezo wa kuzima moto hadi kwenye jengo lenye ghorofa 12, lakini pia lina uwezo wa kubeba maji lita 5000 sawa na tani tano na kuna vifaa vyote muhimu na vya kisasa ambavyo vinawezesha shughuli za kuzimamoto na uokoaji kufanyika kwa ufanisi.
“kama kuna tukio la Moto na kwenye hilo tukio kuna mtu wa kumuokoa kabla ya kuzima moto, mtambo huu unavyo vifaa vya kufanya uokoaji huo kwanza na baadaye tukaendelea na zoezi la kuzima moto na hata kama eneo hilo ni finyu au limezungukwa na vyuma vipo vifaa vya kupamba na hali hiyo,” alisema Mtitu.
KAIMU Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Simiyu, Faustine Mtitu akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi Mtambo wa Zimamoto na Uokoaji wilaya ya Busega.Aidha, Kamanda Mtitu anabainisha kuwa uwekezaji huo ni sehemu ya jitihada za Serikali katika kuhakikisha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji linakuwa na vifaa vya kisasa, ambapo katika Mkoa wa Simiyu Wilaya zote tano zimepatiwa mitambo hiyo ya kisasa.
Mkuu wa Wilaya hiyo Faiza Salum anasema kuwa ujio wa mtambo huo unaonyesha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ya kuendelea kuboresha usalama wa wananchi kwa kuimarisha huduma za dharura nchini.
Faiza ameishukuru serikali pamoja na jeshi la Zimamoto kuipatia Wilaya yake mtambo huo, huku akilitaka Jeshi hilo katika Wilaya hiyo kuhakikisha mtambo huo unatunzwa na kutumika kwa ufanisi ili uweze kudumu kwa muda mrefu na kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi.
Mkuu wa Wilaya hiyo Faiza Salum akizungumza kwenye hafla ya kukabidhiwa Mtambo wa kisasa wa Zimamoto na Uokoaji.Baadhi ya wananchi wa wilaya hiyo walieleza kufurahishwa na hatua ya Serikali kupeleka huduma hiyo muhimu karibu nao, wakisema itarahisisha upatikanaji wa huduma za zimamoto na uokoaji kwa wakati tofauti na ilivyokuwa hapo awali.
Akizungumza kwa niaba yao, Kulwa Ngololo mkazi wa Nyashimo, alisema awali walilazimika kutegemea huduma kutoka Wilaya ya Magu mkoani Mwanza, hali iliyokuwa ikisababisha ucheleweshaji wa huduma wakati wa majanga.
Hii ni mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa Mkoa wa Simiyu Mwaka 2012, Wilaya ya Busega inapatiwa Mtambo wa kisasa wa kupambana na majanga ya moto na uokoaji ikiwa ni juhudi za serikali katika kuboresha huduma kwa Jeshi Zimamoto na Uokoaji nchini.
Mwisho.



0 Comments