Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Maswa, Maisha Mtipa akizungumza katika kikao cha baraza la madiwani.Na Samwel Mwanga,Maswa.
MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu, Maisha Mtipa amewataka watendaji wa kata kuhakikisha taarifa wanazowasilisha kwenye vikao vya baraza la madiwani zinaonyesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayofanywa na serikali katika maeneo yao.
Akizungumza katika kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Maswa wakati wa usomaji wa taarifa za kata, Mtipa amesema kuwa taarifa nyingi zimekuwa zikijikita zaidi kwenye changamoto zinazokabili maeneo hayo huku zikisahau kueleza mafanikio na miradi iliyotekelezwa kwa kipindi husika.
Alisema ni muhimu kwa watendaji hao kuonyesha wananchi na viongozi hatua zinazochukuliwa na serikali katika kuboresha huduma za kijamii na maendeleo ya wananchi kupitia miradi mbalimbali inayotekelezwa katika kata zao.
“Ni vizuri taarifa hizi zikaonyesha pia miradi ya maendeleo iliyotekelezwa na serikali katika kipindi husika badala ya kueleza changamoto pekee. Wananchi wanahitaji kuona kazi zinazofanywa na serikali yao,” amesema Mtipa.
Aidha, aliwataka watendaji hao kuhakikisha wanatoa taarifa zenye uwiano kwa kueleza mafanikio yaliyopatikana pamoja na changamoto zilizopo ili kuwezesha baraza kupata picha halisi ya maendeleo katika maeneo yao.
Taarifa zinazobeba mafanikio ya utekelezaji wa miradi husaidia kuongeza uwazi na kuwapa wananchi uelewa wa namna fedha za serikali zinavyotumika katika kuwaletea maendeleo.
Mwisho.
0 Comments