Na Mwandishi wetu.
KATIBU Tawala Mkoa wa Simiyu, Prisca Kayombo, amefungua kikao kazi kuhusu utekelezaji wa Programu ya SCALE ya kukabiliana na mabadiliko ya Tabia Nchi inayohusu uboreshaji wa mazingira Mkoani Simiyu.
Imeelezwa kuwa Utekelezaji wa Mradi huo unalenga kujenga uwezo kwa jamii ya Mkoa huo kukabiliana na mabadiliko ya Tabia Nchi.
Mafunzo hayo ambayo yaliyofadhiliwa na Benki ya Dunia, na kuratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) yamefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Nyaumata, Wilayani Bariadi.
Akizungumza na Waratibu ngazi ya Mkoa na Halmashauri waliohudhuria mafunzo hayo, Katibu Tawala Kayombo amewataka kutekeleza kwa weledi Programu hiyo ili kufikia malengo mahsusi ya Serikali katika kuboresha mazingira.
Amewahakikishia waratibu wa Programu hiyo kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI kuwa Serikali Mkoani Simiyu itashirikiana nao bega kwa bega kufanikisha utekelezaji wa programu hiyo.
Mkoani Simiyu Programu ya Scale inatekelezwa katika Halmashauri mbili ambazo ni Maswa na Meatu ambapo katika ngazi ya Taifa Programu hiyo inatekelezwa katika mikoa 21 na Halmashauri 54 za Tanzania bara.
Mwisho.






0 Comments