DC SIMALENGA AZINDUA ZOEZI LA UANDIKISHAJI VITAMBULISHO VYA NIDA VIJIJINI.

MKUU wa Wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu, Simon Simalenga (kushoto) akishiriki kuona namna ya usajili wa vitambulisho vya Taifa (NIDA) ilivyokuwa unafanyika katika kijiji cha Ikungulyabashahi wilayani Bariadi.

Na Mwandishi wetu.

MKUU wa Wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu, Simon Simalenga, amezindua rasmi zoezi la Uandikishaji wa vitambulisho vya Taifa (NIDA) vijijini, huku akiwahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki zoezi hilo muhimu la kitaifa.

Akizungumza katika uzinduzi huo uliofanyika leo katika Kijiji cha Ikungulyabashahi wilayani humo, Simalenga amesisitiza umuhimu wa kila mwananchi kuwa na kitambulisho cha Taifa, na kutoa wito kwa jamii kushirikiana na mamlaka husika kubaini na kufichua watu wasio raia wanaojaribu kujipenyeza katika zoezi hilo.


Kwa upande wake, Afisa Usajili wa Mkoa, Ohana Ngotolainyo, amesema zoezi hilo lilianza rasmi Aprili 24, 2026, na linatarajiwa kukamilika Mei 20, 2026. Amewahimiza wananchi wote wanaostahili kutumia fursa hiyo kabla ya muda kuisha.

Baadhi ya wananchi kutoka ikungulyabashashi akiwemo Yohana Misese na Aisha Ramadhani wameipongeza serikali kwa kusogeza huduma hiyo karibu zaidi na makazi yao huku wakieleza kuwa hapo awali walilazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hiyo muhimu.

Mwisho.







Post a Comment

0 Comments