William Mataba mtaalamu wa malisho ya mifugo kutoka shamba la Sao Hill mkoani Iringa akiwaelezea baadhi ya wafugaji wa mkoa wa Simiyu juu ya matumizi ya mbegu za malisho katika shamba la mfano la malishio ya mifugo la Masela wilaya ya Maswa mkoani Simiyu.
Samwel Mwanga Maswa.
WAFUGAJI katika mkoa wa Simiyu wametakiwa kuwekeza katika mashamba ya malisho kwani ni msingi muhimu wa mafanikio ya ufugaji kwa afya bora ya mifugo na uzalishaji wa maziwa katika upatikanaji wa lishe bora.
Akizungumza April 21,2026, William Mataba kutoka shamba la kuzalisha mitala la Sao Hill, kitengo cha malisho biashara alipotembelea shamba la mfano la mbegu za malisho ya mifugo katika kijiji cha Masela wilaya ya Maswa amesema kuwa kwa sasa serikali kupitia kwa wadau mbalimbali wanahamasisha wafugaji kuwa mashamba hayo.
Amesema kuwa katika mkoa huo kupitia mradi wa mabadiliko ya tabia nchi ambao unatekekezwa kwa kipindi cha miaka mitatu wanawahamasisha wafugaji kubadili mtazamo ili waweze kufuga kisasa mifugo wachache kwa kuwapatia malisho bora.
Sehemu ya shamba la mfano la malisho ya mifugo katika kijiji cha Masela wilaya ya Maswa lililotembelewa na wafugaji wa mkoa wa Simiyu walioko kwenye Mradi wa Mabadiliko ya tabia nchi Simiyu."Ni lazima tubadili mtazamo wa mfugaji mmoja mmoja hadi ngazi ya taifa tunahitaji wafugaji wetu wafuge mifugo michache na waweze kuihudumia ili wapate tija na moja wapo wa eneo hili ni kila mfugaji kuwa na shamba lake la malisho ya mifugo," amesema.
Amesema kuwa serikali itaendelea kugawa mbegu za malisho hayo sambamba na kuanzisha mashamba ya mifano ili wafugaji waweze kujifunza kwa lengo pia la utunzaji wa mazingira na kurejesha uoto wa asili.
Basu Kayungilo ni mfugaji kutoka kijiji cha Mwandoya wilaya ya Meatu amesema kuwa kukosekana kwa maeneo maalum ya malisho kunasababisha mifugo kudhoofika na wakati mwingine kufa hali inayosababisha hasara kubwa kwa wafugaji.
“Shamba la malisho ni kama benki yetu. Tukililinda na kulitunza vizuri, mifugo yetu inakuwa na afya, inatoa maziwa mengi na hata uzazi unaongezeka,” alisema.
Kwa upande wake, Specioza Mikaeli kutoka kijiji cha Manala wilaya ya Busega amesema kuwa wafugaji wengi bado hawajazingatia umuhimu wa kuandaa mashamba maalum ya malisho, badala yake wanategemea malisho ya asili ambayo hupungua sana wakati wa kiangazi.
"Serikali za mitaa zitenge maeneo rasmi kwa ajili ya malisho na kutoa elimu kwa wafugaji kuhusu mbinu bora za ufugaji wa kisasa,"amesema.
Naye Limi Kulwa wa kijiji cha Shishiyu wilaya ya Maswa amesema kuwa ni muhimu kwa wafugaji kupanda nyasi bora na kuhifadhi malisho kwa ajili ya matumizi ya baadaye ili kukabiliana na upungufu wa chakula kwa mifugo.
“Lishe duni husababisha mifugo kushindwa kuzalisha ipasavyo, hivyo mfugaji hupata hasara. Ndiyo maana serikali inatusisitiza tufanye uwekezaji katika mashamba ya malisho,” amesema.
Mkuu wa wilaya ya Maswa, Dk Vicent Naano amesema kuwa huu ni wakati wa viongozi na wataalam kusaidia kuwabadilisha mtazamo wananchi hasa wafugaji waweze kufuga kisasa.
Mkuu wa wilaya ya Maswa, Dk Vicent Naano akiongea na wafugaji wa mkoa wa Simiyu walioko katika mradi wa mabadiliko ya tabia nchi Simiyu juu umuhimu wa kuwa na mashamba malisho ya mifugo.Pia ametoa wito kwa wadau wote kushirikiana kuhakikisha upatikanaji wa malisho unakuwa wa uhakika, ili kuimarisha sekta ya mifugo na kuchangia maendeleo ya uchumi wa kaya na taifa kwa ujumla.
"Tuwe sehemu ya mabadiliko kwa wana Simiyu,mabadiliko yanawezekana tukiamua,tunaze na mtu mmoja mmoja na tukufanya hivyi kwa wakulima na wafugaji,umasikini unaondoka wenyewe,"amesema.
Mwisho.



0 Comments