SERIKALI YATENGA SHILINGI MIL. 408.9 UJENZI NYUMBA YA DC MASWA.

 

Mkuu wa wilaya ya Maswa,Dkt Vicent Naano Anney (aliyekati) akizungumza kwenye eneo ambalo itajengwa nyumba mpya ya makazi ya Mkuu wa wilaya hiyo.

Na Samwel Mwanga, Maswa

SERIKALI imetenga kiasi cha shilingi Milioni 408.9 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba mpya ya makazi ya Mkuu wa Wilaya ya Maswa, mradi unaotarajiwa kukamilika ndani ya miezi minne.

Taarifa hiyo imetolewa Aprili 30, 2026 na Mhandisi Boniface William kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu wakati wa makabidhiano ya eneo la ujenzi kwa mkandarasi Kampuni ya Equiplus ya Jijini Dar Es Salaam,mjini Maswa, eneo lililokuwa likitumika kama makazi ya zamani ya Mkuu wa wilaya hiyo.

Makabidhiano hayo yalishuhudiwa na Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dkt. Vicent Naano Anney, pamoja na baadhi ya viongozi na watendaji wa serikali mkoani Simiyu.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mhandisi William amesema ujenzi wa nyumba hiyo ni sehemu ya juhudi za serikali kuboresha mazingira ya kazi kwa viongozi wake ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

Alifafanua kuwa jengo hilo litajengwa kwa kuzingatia hadhi ya Mkuu wa Wilaya, likiwa na viwango vinavyostahili ili kuhakikisha kiongozi huyo anaishi katika mazingira bora na salama.

Mhandisi Boniface William kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu akizungumza wakati wa makabidhiano ya eneo la ujenzi kwa mkandarasi Kampuni ya Equiplus ya Jijini Dar Es Salaam,mjini Maswa, 

“Tunayo furaha kwa serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kutupatia fedha hizi kwa ajili ya ujenzi huu. Sasa jukumu kubwa lipo kwa mkandarasi kuhakikisha anakamilisha kazi kwa wakati ili Mkuu wa Wilaya aweze kuishi katika mazingira mazuri na kuwatumikia wananchi wa Maswa ipasavyo,” amesema.

Kwa upande wake, Mhandisi Shaban Ibrahim kutoka Equiplus Company Ltd ya jijini Dar es Salaam, iliyoshinda zabuni ya utekelezaji wa mradi huo, alisema tayari wamepokea eneo la ujenzi na wako tayari kuanza kazi mara moja.

Alisema kwa mujibu wa mkataba, ujenzi huo unatakiwa kukamilika ndani ya miezi minne, lakini kampuni yake imelenga kuukamilisha ndani ya miezi miwili bila kuathiri ubora wa kazi.

“Tumekabidhiwa eneo la ujenzi leo na tumejipanga kuhakikisha tunatekeleza mradi huu kwa viwango vya juu. Ingawa mkataba unatupa miezi minne, tutajitahidi kuukamilisha ndani ya miezi miwili kwa ubora uliotukuka,” amesema.

Mhandisi Shaban Ibrahim kutoka Equiplus Company Ltd ya jijini Dar es Salaam, iliyoshinda zabuni ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa nyumba ya makazi ya Mkuu wa wilaya ya Maswa akizungumza mara baada ya kuonyeshwa eneo la ujenzi.

Mkuu wa wilaya ya Maswa, Dkt Vicent Naano Anney amesema kuwa atazungumza zaidi pindi ujenzi utakapoanza kutekekezwa ila amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kukubali kuidhinisha pesa hizo kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya makazi ya Mkuu wa wilaya hiyo.

Hata hivyo, baadhi ya wananchi wa Maswa wametoa maoni tofauti kuhusu utekelezaji wa mradi huo, wakieleza matarajio yao kwa serikali.

Naye mama lishe, Rehema Magesa amesema anatarajia uwepo wa makazi bora kwa Mkuu wa Wilaya utaongeza uwajibikaji katika kuwahudumia wananchi.

“Kiongozi akiwa na mazingira mazuri ya kuishi anaweza kufanya kazi kwa utulivu zaidi. Tunategemea kuona matokeo chanya kwa wananchi,” amesema.

Kwa upande wake, mkulima kutoka kijiji cha Iyogelo, Paulo Shilinde alisisitiza umuhimu wa usimamizi wa karibu wa mradi huo ili kuhakikisha thamani ya fedha inapatikana.

“Miradi mingi huwa inachelewa au haikamiliki kwa ubora unaotakiwa. Tunaomba ujenzi huu usimamiwe vizuri ili fedha ya serikali isipotee,” amesema.

Mradi huo unatarajiwa kuongeza hadhi ya ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Maswa pamoja na kuboresha mazingira ya utendaji kazi, hali itakayomuwezesha kiongozi huyo kuwatumikia wananchi kwa ufanisi zaidi.

Mwisho.



Post a Comment

0 Comments