SERIKALI Kupitia ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, imesema ipo katika hatua za kuanza ujenzi wa soko la kisasa la mnada wa mifugo katika Wilaya ya Meatu Mkoani Simiyu, hatua inayolenga kuboresha mazingira ya biashara ya mifugo na kuongeza mapato ya halmashauri.
Kauli hiyo imetolewa leo Aprili 24, 2026 Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI, Dk. Festo Dugange, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Meatu, Salum Khamis Salum, aliyetaka kujua ni lini serikali itaanza ujenzi wa Soko la Mnada wa Mifugo katika Jimbo la Meatu.
Akijibu swali hilo, Dk. Dugange amesema Halmashauri ya Wilaya ya Meatu ina minada minne ya awali ambayo ni Bukundi, Itinje, Mwanhuzi na Tindabuligi, lakini inahitaji kuboreshwa ili kukidhi mahitaji ya sasa.
Amesisitiza kuwa, serikali inatambua umuhimu wa kuboresha miundombinu hiyo ili kuweka mazingira rafiki kwa wafugaji na wanunuzi.
Amefafanua kuwa, katika mwaka wa fedha 2023/24, halmashauri ilitumia shilingi milioni 14.3 kutoka mapato ya ndani kwa ajili ya kuboresha machinjio, vyoo na kutenga eneo la ekari nane kwa ajili ya mnada wa kisasa katika Kijiji cha Bukundi.
Aidha, Dk. Dugange amebainisha kuwa, katika mwaka wa fedha 2025/26, halmashauri ilitenga shilingi milioni 12 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa awamu ya kwanza ya uzio wa mnada huo na kwamba, ujenzi huo kuanza mwezi Mei 2026 huku taratibu nyingine za upatikanaji wa fedha za ujenzi wa soko zikiendelea kukamilishwa.
Source..
#uhuruonline.


0 Comments