MKURUGENZI MPYA MAUWASA AAHIDI USHIRIKIANO MASWA.

 


Na Samwel Mwanga,Maswa.

Mkurugenzi Mtendaji mpya wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Maswa (MAUWASA), Poas Kilangi(mwenye suti nyeusi) leo amewasili rasmi katika ofisi za mamlaka hiyo mjini Maswa na kuanza kujitambulisha kwa wafanyakazi wake, huku akitarajia kuanza majukumu rasmi mara baada ya kukabidhiwa ofisi.

Katika ziara hiyo ya awali, Kilangi alifanya mazungumzo na watumishi wa MAUWASA pamoja na kutembelea Ofisi za Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Maswa, ambako alikutana na Katibu wa CCM Wilaya, Mwl. Efreim Kolimba.

Mbali na hilo, alikutana na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa MAUWASA, Faustine Makeja, Mwakilishi wa Meneja wa RUWASA Wilaya ya Maswa, Wilson Magaigwa, pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dkt. Vicent Naano Anney, akiwa pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya.

Akizungumza baada ya utambulisho huo, Kilangi aliahidi kushirikiana kwa karibu na wadau wote ili kuhakikisha huduma ya maji safi na salama inaimarika zaidi wilayani humo.

Alisema ataendeleza mafanikio yaliyopatikana chini ya mtangulizi wake, Mhandisi Nandi Mathias, aliyehamishiwa katika Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Bariadi (BARUWASA), huku akisisitiza dhamira yake ya “kumtua mama ndoo kichwani” kwa kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi.

Kabla ya uteuzi wake, Kilangi alikuwa akihudumu katika Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Kigoma Mjini, ambako alipata uzoefu unaotarajiwa kusaidia kuboresha huduma za maji katika Wilaya ya Maswa.

Mwisho.










Post a Comment

0 Comments