Mkuu wa wilaya ya Maswa, Dk Vicent Naano akiongea na viongozi na watendaji wa wilaya hiyo katika mkutano wa pamoja uliowakutanisha kwa ajili ya kupeana elimu ya utekekezaji wa majukumu.Picha na Samwel Mwanga.
Samwel Mwanga,Maswa.
MKUU wa Wilaya ya Maswa, Dkt Vicent Naano amewataka viongozi wa kisiasa na watendaji wa serikali katika wilaya hiyo kufanya kazi kwa mshikamano huku kila mmoja akizingatia mipaka ya majukumu yake ili kuharakisha maendeleo ya wananchi.
Akizungumza Machi 29, 2026 katika mkutano wa pamoja wa viongozi na watendaji uliofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, amesema kuwa changamoto kubwa aliyoibaini ni mwingiliano wa majukumu unaosababisha kucheleweshwa kwa utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Amesema katika ziara zake vijijini amekutana na hali ya viongozi kuingiliana majukumu, jambo linalosababisha mkanganyiko na kushusha ufanisi wa utendaji kazi.
“Wakati wa ziara yangu nimekuta kuna makundi kati ya viongozi na watendaji. Diwani anataka kufanya kazi za mtendaji wa kata, mwenyekiti wa kijiji anataka kufanya kazi za diwani, na mtendaji naye anataka kufanya kazi ya diwani hili ni tatizo,” amesema .
Aliongeza kuwa iwapo kila kiongozi atatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria na taratibu, utekelezaji wa shughuli za maendeleo utakwenda kwa ufanisi zaidi.
Amesema wilaya hiyo bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo upungufu wa madawati shuleni na lishe duni kwa watoto, hali inayochangia udumavu unaofikia asilimia 30.
“Changamoto hizi haziwezi kutatuliwa kama hatutakuwa na mshikamano na nidhamu ya uongozi katika kutekeleza majukumu ya serikali,” amesema.
Baadhi ya viongozi na watendaji wa wilaya ya Maswa wakiwa kwenye mkutano wa pamoja.Picha na Samwel Mwanga.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyabubinza,Juma Sabasaba amesema mwingiliano huo umekuwa ukisababisha mkanganyiko kwa wananchi na watendaji.
“Tunapanga mipango ya kijiji kwa kushirikiana na watendaji, lakini diwani anaingilia na kutoa maelekezo tofauti. Hii inasababisha wananchi na watendaji kushindwa kujua wa kufuata nani,” amesema.
Ameongeza kuwa hali hiyo imekuwa ikichelewesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ikiwemo ya elimu na afya.
“Maamuzi yanayofanyika kwenye vikao halali yanabadilishwa bila utaratibu, mwisho wa siku miradi inasimama au kuchelewa,” amesema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Shinyangamwenge,Deus Mikembo amesema changamoto hiyo imekuwa ikiwavunja moyo viongozi wa ngazi ya kijiji.
“Kuna wakati unahisi kama huna mamlaka kabisa. Diwani anaweza kuja na kuamua jambo bila kushirikisha uongozi wa kijiji, wakati sisi ndio tunaowajibika moja kwa moja kwa wananchi,” amesema.
Ameeleza kuwa hali hiyo imekuwa chanzo cha migogoro isiyo ya lazima kati ya viongozi na watendaji.
“Badala ya kushirikiana, tunaingia kwenye mvutano usio na tija. Mwisho wa siku huduma zinachelewa au kutotolewa kabisa,” ameongeza.
Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Mbaragane,Mbuli Mageni amesema suluhisho la changamoto hiyo ni kila kiongozi kuheshimu mipaka ya madaraka yake.
“Kila mmoja ana jukumu lake kisheria. Tatizo linakuja pale mtu anapotaka kufanya kazi ambayo si yake, na hii inaleta sintofahamu katika utekelezaji wa maamuzi ya serikali,” amesema.
Ameonya kuwa iwapo hali hiyo haitadhibitiwa, malengo ya maendeleo ya vijiji yatakuwa magumu kufikiwa.
“Tunahitaji nidhamu ya uongozi na usimamizi madhubuti ili kila mmoja awajibike kwenye nafasi yake,” amesema.
Mwisho



0 Comments