Na Samwel Mwanga, Maswa.
MKUU wa Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu, Dk Vicent Naano ameongeza kasi ya kampeni ya kuhakikisha wanafunzi wanapata chakula shuleni, akisema mpango huo si wa kuboresha ufaulu pekee bali pia ni sehemu ya mapambano dhidi ya udumavu wa watoto unaotokana na lishe duni.
Dk. Naano amesema takwimu zinaonyesha asilimia 30 ya watoto katika wilaya hiyo wanakabiliwa na tatizo la udumavu, hali inayotishia afya, ukuaji na maendeleo yao ya kielimu.
Akizungumza katika mikutano ya uhamasishaji kwa wazazi na jamii katika vijiji vya Kadoto na Mwanghonoli amesema suluhisho la changamoto hiyo linaanzia kwenye ushiriki wa wazazi kuchangia chakula cha watoto wao mashuleni.
“Chakula cha mchana ambacho angekula mtoto nyumbani sasa tukihamishie shuleni,” amesema.
Katika utekelezaji wa kampeni hiyo, wazazi wa kila mwanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani humo wametakiwa kuchangia madebe matatu ya mahindi na kilo sita za maharage kwa mwaka, chakula kitakachotumika kuandaa milo ya wanafunzi wakiwa shuleni.
Amesema kuwa uwepo wa chakula shuleni utasaidia kuongeza umakini wa wanafunzi darasani, kupunguza utoro na kuinua ufaulu, huku pia ukisaidia kukabiliana na athari za lishe duni.
Baadhi ya shule wilayani humo tayari zimeanza kuona matokeo ya mpango huo, zikiripoti kuongezeka kwa mahudhurio ya wanafunzi na kupungua kwa tabia ya watoto kurudi nyumbani mchana kutafuta chakula.
Wazazi mbalimbali wameonyesha kuunga mkono kampeni hiyo wakisema ni hatua muhimu kwa mustakabali wa watoto wao.
Neema Magesa, mkazi wa kijiji cha Malampaka amesema awali baadhi ya wazazi waliona mchango huo kama mzigo, lakini elimu iliyotolewa imewafanya waone umuhimu wake.
“Ukitoa hayo mahindi na maharage si hasara, ni uwekezaji kwa mtoto. Mtoto akiwa ameshiba anasoma vizuri,” amesema.
Naye Michael Mgogo wa Sola mjini Maswa amesema mpango huo utasaidia hata familia zenye changamoto za kipato kuhakikisha watoto hawakai njaa wakiwa shuleni.
“Bora chakula kiwe shuleni kuliko mtoto akateseke siku nzima. Hili jambo lina tija kwa elimu na afya,” amesema.
Kwa upande wake Vumilia Masanja mzazi wa mwanafunzi wa shule ya msingi Shishiyu anasema kampeni hiyo imewafanya wazazi watambue kuwa malezi na elimu vinaenda pamoja.
“Tulizoea kuiona shule kazi ya walimu pekee, lakini sasa tunaona nasi tuna wajibu wa kuchangia maendeleo ya watoto wetu,” amesema.
Sehemu ya wazazi katika kijiji cha Mwasita wilaya ya Maswa ambao walijitokeza kusikiliza mkutano wa Mkuu wa wilaya hiyo,Dk Vicent Naano(hayupo pichani)wakati wa kampeni ya lishe kwa wanafunzi shuleni wilayani humo.Picha na Samwel Mwanga.Jerry Nyabululu ni mdai wa elimu wilayani humo anasema mpango wa chakula shuleni unaweza kuwa nyenzo muhimu ya kupunguza udumavu huku ukiimarisha matokeo ya kitaaluma, hasa katika maeneo ya vijijini.
"Kampeni ya Dk Naano inaweza kuwa mfano wa kuigwa katika wilaya nyingine maana kuunganisha lishe na elimu ni mkakati unaogusa changamoto mbili kwa wakati mmoja," amesema.
Kadri kampeni hiyo inavyoendelea kushika kasi, matarajio ni kuona ushiriki wa wazazi ukiongezeka zaidi ili shule ziwe sio tu vituo vya kujifunza, bali pia maeneo salama ya kulea watoto wenye afya, maarifa na ndoto za kesho.
Mwisho.


0 Comments